Mwandishi:
Mhhariri
ULYCLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Alhamisi, 1 Julai 2021
Saratani
Kufahamu saratani ni nini ni vema kwanza kufahamu kuwa mwili wa binadamu umetengenezwa kwa chembe hai zenye uwezo wa kuzaliana, kukua na kufa mara zinapozeeka au zinapopoteza uwezo wake wa kufanya kazi. Utaratibu huu ni wa asili na huongozwa na vimeng’enya maalumu vilivyo ndani ya chembe hai ambayo hurithiwa kwenye jeni. Endapo jeni ya chembe moja itabadili utaratibu huu kutokana na sababu yoyote na kuanza kuzalina kwa haraka, kuishi bila kufa na kutengeneza uvimbe sehemu husika ya mwili hii husababishwa kutokea kwa saratani.
Dalili
Kama ilivyo kawaida ya magonjwa mengine kutoonesha dalili za haraka mwanzoni, vivyo hivyo dalili za saratani ni vigumu kuonekana mara inapoanza na hivyo kufanya kuwa rahisi kuchelewa kutambuliwa.
Endapo dalili zitaanza kuonekana, zitategemea sehemu saratani ilipo au sehemu imejipandikiza baada kusambaa na huongezeka kwa jinsi tatizo linavyozidi kuwa kubwa.
Dalili za saratani zinajumuisha;
Uchovu mkali
Uvimbe eneo ambapo kuna ssaratani
Kupungua uzzito bila sababu
Mabadiliko ya ngozi kama vile kuwa nyeusi zaidi au nyekundu zaidi n.k
Mabadiliko ya tabia ya tumbo
Kukohoa endelevu au kukuhoa damu
Mabadiliko ya tabia ya kukojoa
Kushindwa kumeza chakula
Kukwa ma kwa sauti ( sauti ya farasi)
Kutokwa na damu ukeni
Difficulty swallowing
Kutokwa na damu bila sababu
Maambukizi ya mara kwa mara
Maumivu ya viungo yasiyo na sababu
Visababishi
Saratani husababishwa na mabadiliko yanayotokea kwenye jeni ya seli, ambayo hupelekea seli kupoteza uwezo wake wa kujizalisha, kukua na kufa kwa utaratibu wake wa awali.
Ni nini husababishwa mabadiliko ya jeni za chembe hai?
Mabadiliko ya kuzaliwa nayo. Haya hurithiwa kutoka kwa wazazi, saratani aina hii hutokea kwa asilimia chache.
Mabadiliko ya jeni baada ya kuzaliwa
Mabadiliko ya jeni husababishwa na;
Uvutaji wa sigara
Kupigwa na mionzi
Maambukizi ya virusi
Matumizi ya kemikali zinaofahamika kuwa kasinojeni
Uzito uliokithiri
Michomo sugu ya kinga za mwili
Kutofanya mazoezi
Aina za saratani
Saratani inaweza kujitokeza sehemu yoyote ile ya mwili wa binadamu, sehemu saratani ilipo au aina ya tishu zilizoathiriwa huipa jina la saratani. Mfano wa saratani zinazotokea ni saratani ya;
Damu
Ini
Kibofu cha mkojo
Kongosho
Koo
Macho
Mapafu
Matiti
Mifupa
Misuli
Ngozi
Shingo ya kizazi (seviksi)
Tezi dume
Tezi limfu
Tumbo
Ubongo
Utumbo
Vihatarishi
Mara nyingi haifahamiki ni nini kinatokea hadi chembe hai kuwa na tabia isiyo ya kawaida na kuleta saratani. Wanasayansi wameona kuwa kuna mchanganyiko wa mambo mengi ambayo kwa pamoja yanaweza kupelekea kupata saratani. Licha ya sababu kutofahamika, vipo vihatarishi vinavyofahamika kusababisha saratani endapo mtu atakuwa navyo ambavyo ni;
Matumizi ya kemikali kali
Kupigwa na mionzi
Uvutaji wa sigara
Maambukizi ya virusi virus , bacteria na fangasi
Matumizi ya pombe kupindukia
Ulaji wa vyakula vya mafuta mengi
Ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi
Kutofanya mazoezi
Unene uliokithiri
Matumizi ya dawa mbalimbli au viua wadudu
Kuanza ngono kwenye umri mdogo au kuwa na wapenzi wengi
Chembe za saratani zinaweza sambaa?
Chembe za saratani zinauwezo wa kusafiri kutoka sehemu moja ya mwili kwenda nyingine kwa kupitia;
Njia ya damu
Njia ya limfu
Njia ya kupenyeza chembe jirani
Saratani inaambukizwa?
Hapana! Saratani haiambukizwi
Vipimo na utambuzi
Saratani hutambuiwa kwa njia tofauti zikiwa pamoja na;
Uchunguzi wa mwili wako na daktari
Daktari atchunguza uvimbe baada ya kuchukua historia ya tatizo lako kwa kutumia mikono au vifaa mbalimbali vya kitaalamu ili kutambua kama una saratani na sifa zake.
Vipimo vya picha ya mionzi
Vipimo hivi hufanyika kutambua aina na sifa za saratani na maeneo ambapo saratani imesambaa vipimo hivyo hujumuisha
Computerized tomography (CT) scan,
Bone scan,
Magnetic resonance imaging (MRI)
Positron emission tomography (PET) scan
Ultrasound
X-ray
Na vingine
Kipimo cha biopsy
Chembe za saratani zitachukuliwa kwa ajili ya kutizama uwepo wa saratani kwenye chembe hizo maabara, hii ni njia pekee inayoweza kusema kutofautisha uvimbe wa kawaida na saratani. Utambuzi wa saratani kwa njia hii hutumia kuangalia sifa za chembe za saratani na sehemu zilipotoka, endapo chembe zitaonekana kuwa zina maumbile tofauti ya sehemu zilipotoka na hazina mpangilio mzuri, chembe hizi huwa na sifa ya saratani.
Vipimo vya maabara
Vipimo vya mkojo na damu hufanyika kwa lengo la kutambua saratani au madhara ya saratani. Mfano wa vipimo ni FBP ambacho hufanyika sana kwa wagonjwa wenye saratani ya damu.
Matibabu
Matibabu ya saratani yapo ya aina nyingi ikitegemea aina ya saratani na mahali ilipo katika mwili. Daktari anaweza kupendekeza matumizi ya tiba moja au zaidi ya moja, na huhusisha;
Upasuaji wa kuondoa uvimbe au sehemu ya uvimbe
Dawa za chemotherapi
Tiba ya kutumia Mionzi kuua chembe za saratani
Tiba ya vichochezi au homoni
Tiba dhamiria- hulenga kutambua udhaifu wa chembe za saratani unaofanya chembe iwe na tabia za kisaratani kisha kuzuia
Tiba ya jeni- hulenga kutambua udhaifu wa jeni
Tiba ya stem seli
Tiba majaribio- hizi ni tafiti zinazolenga kugundua dawa mpya za saratani, kuna tafiti nyingi zinaendelea duniani kudungua njia nzuri na mpya za matibabu ya saratani.
Tiba mbadala ya saratani
Hakuna tiba mbadala (tiba asilia) ambayo imethibitishwa kutibu saratani, hata hivyo kuna baadhi ya dawa asili zimeonekana kutibu saratani na baadhi ya wagonjwa wamepona kwa kutumia tiba hizo. Unapokuwa unatumia tiba mbadala unatakiwa kushauriana na daktari wako kwanza kuhusu mwingiliano wa tiba hizo na dawa za hospitali.
Kuna matibabu ya kuponya saratani?
Jibu la swali hili kwa sasa ni hapana, hii ni kwa sababu hakuna tiba mpaka sasa iliyothibitishwa kuponya saratani kabisa. Hata hivyo kuna matibabu ya kupunguza au kudhibiti saratani na endapo itagunduliwa mapema kwenye hatua za awali kabisa, mwathirika anaweza kupona na hivyo kuishi na kufa na magonjwa mengine yasiyohusiana na saratani kama watu wengine.
Matibabu mengi yaliyopo hayaponyi saratani bali humponya mtu kwenye madhara ya saratani lakini saratani huendelea kuwa kisababishi cha kifo kwa waathirika haswa endapo waligunduliwa kwa kuchelewa.
Kinga
Baadhi ya saratani ambazo zinazofahamika visababishi vyake huweza zuilika kwa kufanya mamb yafuatayo;
Acha kuvuta sigara
Kama unavuta sigara unapaswa kuacha ili kujikinga na saratani ya mapafu na zingine zinazotokana na uvutaji wa sigara.
Jikinge na kupigwa na mwanga wa jua kupita kiasi
Mwanga wa jua una mionzi ambayo inaweza kupelekea kupata saratani ya ngozi. Kaa kwenye kimvuli muda mwingi au kuvaa nguo au kupaka mafuta ya kukukinga na mionzi haswa endapo una ualbino
Kula mlo wa kiafya
Kula mlo kamili wa kiafya unaopendekezwa haswa wenye mboga za majani kwa wingi na nafaka zisizokobolewa. Usile nyma yenye mafuta au nyama nyekundu kwa wingi.
Fanya mazoezi
Inashauriwa kufanya mazoezi angalau kwa dakika 30 kwa muda wa siku 3 hadi 4 kwa wiki. Fanya mazoezi ya aerobiki na anaerobic
Kuwa na uzito wa kiafya
Zingatia kuwa na BMI inayoshauriwa kwa kuzingatia mlo na kufanya mazoezi
Kunywa pombe kidogo
Kama umechagua kunyw apombe, kunywa kwa kiasi kidogo kinachoshauriw akiafya kwa siku.
Fanya uchunguzi wa saratani
Ongea na daktari wako akufahamishe unatakiwa kuanya uchunguzi wa saratani gani kulingana na kihatarishi ulichonacho.
Pata chanjo ya saratani zilizopo
Kuna chanjo nyingi zipo kama vile chanjo ya kirusi cha homa ya ini B (HBV) anayesababisha saratani ya ini, kirusi cha human papillomavirus (HPV) anayesababisha saratani ya shingo ya uzazi na koo na zingine.