Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Benjamin L, MD
Dkt. Salome A, MD
Jumamosi, 3 Agosti 2024
Ugonjwa wa Mpox
Mpox ni ugonjwa unaotokea kwa nadra na husababishwa na kirusi cha mpox. Kirusi hiki mara nyingi huathiri panya na wanyama jamii ya nyani kama vile tumbili, sokwe n.k na wakati mwingine binadamu anaweza kuathiriwa na ugonjwa.
Mpox hutokea maranyingi Afika ya Kati na Magharibi. Endapo ugonjwa ukitokea nnje ya Afrika mara nyingi huwa kwa sababu ya kusafiri kwenda Afrika pamoja na kugusana na wanyana wenye ugonjwa kutoka Afrika.
Mwaka 2022 ugonjwa wa mpox ulianza kuripotiwa katika nchi ambazo hazijawahi kuwa na ugonjwa huo kama vile Marekani na Ulaya.
Â
Dalili za ugonjwa wa Mpox
Dalili za ugonjwa wa mpox huanza siku 3 hadi 7 baada ya kupata maambukizi na hudumu kwa muda wa wiki 2 hadi 4. Dalili hizo ni pamoja na:
Homa
Harara kwenye ngozi (Upele, vidonda na malengelenge)
Kuvimba mitoki
Maumivu ya kichwa
Maumivu ya misuli
Maumivu ya mgongo
Kutetemeka
Uchovu
Â
Harara ya ugonjwa wa mpox
Harara ya mpox huonekana siku 1 hadi 4 baada ya kuanza kupata homa na hutokea kwenye maeneo ya uso, mikono, miguu na huweza kusambaa kwenye maeneo mengine mwili. Wakati mwingine kwa wagonjwa waliopatwa na mpox, harara zilianzia kwneye maeneo ya siri, mdomoni na kooni.
Harara ya ugonjwa wa mpox hupitia hatua mbalimbali kutoka alama tambarare kuwa lenge kubwa na badae hujaa usaha na kutengeneza gamba na kubanduka katika kipindi cha wiki 2 hadi 4. Harara hizi zinaweza kusambaza ugonjwa endapo mtu atagusa.
Â
Uenezaji wa ugonjwa wa Mpox
Kirusi cha mpox husababisha ugonjwa wa mpox. Kirusi hiki husambaa kwa kugusana na mtu au mnyama mwenye ugonjwa huo au kushika kifaa chenye virusi hivyo kama vile shuka, blanketi n.k. Maelezo zaidi yameelezewa hapa chini:
Njia halisi za kusambaza ugonjwa kati ya mtu na mtu ni kama zifuatazo:
Kugusana na mtu mwenye harara, vidonda au majimaji yenye virusi vya mpox katika mwili wake
Kugusa majmaji kutoka kwenye mate, matapishi, jasho na mkojo wa mtu mwenye ugonjwa
Kukaa karibu na mtu mwenye ugonjwa kwa muda mrefu( zaidi ya masaa 4) pamoja na kushiriki naye ngono
Kushika vifaa ambavyo vina virusi vya mpox ( vimetumika na mtu mwenye ugonjwa wa mpox)
Kugusana na matone ya mfumo wa hewa ya mtu mwenye virusi
Kueneza kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto tumboni wakati wa ujauzito
Â
Uenezaji wa ugonjwa wa Mpox kutoka kwa wanyama kuja kwa binadamu
Uenezaji hutokea kwa njia zifuatazo:
Kung’atwa au kukwanguliwa na myama mwenye ugonjwa
Kula nyama ya wanyama poli
Kutumia mazao ya wanyama wenye ugonjwa kama manyoya na ngozi
Kugusana na majimjai au harara ya mnyama mwenye ugonjwa
Kinga dhidi ya ugonjwa wa Mpox
Njia zifuatazo zinaweza kutumika kukinga ugonjwa wa mpox
Usikae karibu na mtu mwenye ugonjwa kwa muda mrefu hasa mwenye harara zinazoelekeana na za ugonjwa wa mpox
Usiguse nguo za mgonjwa mwenye dalili za mpox
Kuwatenga wagonjwa wenye mpox na watu wasio na ugonjwa
Kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka baada ya kugusana na mgonjwa wa mpox au mnyama. Kama maji na sabuni hakuna, tumia kitakasa mikono chenye asili ya kileo
Epuka wanyama ambao wanabeba virusi vya mpox
Chanjo ya ugonjwa wa Mpox
Chanjo ya mpox kama chanjo aina ya ACAM2000 na Jynneos huweza kutumika kukinga ugonjwa wa ndui na mpox. Mtaalamu wa afya huweza kushauri watu waliohatarini kupata chanjo hii. Baadhi ya watu pia wenye hatari ya kupata ugonjwa kama vile wafanyakazi wa maabara wanaweza kushauriwa kupata chanjo hii pia.
Kwa sasa CDC bado haijashauri chanjo kutolewa kwa kila mtu kujikinga na mpox.
Â
Matibabu ya Mpox
Matibabu mara nyingi hulenga kutuliza dalili za ugonjwa. Matibabu yanaweza kuhusisha:
Kutibu uharibifu wa ngozi
Kunywa maji ya kutosha kulainisha haja kubwa
Kutumia dawa za maumivu
Dawa ya matibabu ya kirusi Mpox
Matumizi ya dawa za kirusi cha ndui kama tecovirimat(TPOXX) na  brincidofovir (Tembexa).
Kwa wale ambao hawajaitikia kwenye chanjo, mtaalamu wa afya anaweza kuchoma chanjo ya antibody kutoka kwa mtu ambaye alikuwa na ugonjwa.
Â
Madhara ya ugonjwa wa Mpox
Madhara ya mpox ni pamoja na;
Upofu
Maambukizi mengine
Kifo kwa nadra sana
Magonjwa mengine yenye dalili kama za Mpox
Kuna magonjwa kadhaa yanayoweza kuzalisha dalili za vipele kama vya ugonjwa wa Mpox ambayo ni;
Kaswende
Surua
Tetekuwanga
Ndui
Molluscum contagiosum
Majina mengine ya ugonjwa wa Mpox
Ugonjwa wa Mpox umekuwa ukifahamika pia kama homa ya nyani.
Taarifa ya Tahadhari ya ugonjwa wa Mpox Tanzania
Tarehe 3.08.2024 Wizara ya Afya ilitoa taarifa kuhusu uwepo wa ugonjwa wa mpox katika nchi jirani ya Kenya na kuasa wananchi na wataalamu wa Afya kujihadhari kwa njia zifuatazo:
Kutoa taarifa kupitia namba 199 bila malipo endapo utamuona mtu mwenye dalili za Mpox.
Kuepuka kugusa majimaji ya mwili au ngozi ya mtu mwenye dalili za ugonjwa
Kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kubusiana mtu
mwenye dalili za Mpox.
Kuepuka kugusana na mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox.
Kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Epuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni.
Safisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mhisiwa au mgonjwa pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara.
Kuvaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox.
Kuwahi katika vituo vya huduma za afya unapoona dalili za ugonjwa wa Mpox.
Watoa huduma za afya kuzingatia miongozo ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi (IPC) wakati wote wanapowahudumia wagonjwa.