Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Ijumaa, 18 Juni 2021
Vajinosis ya bakteria (VB)
Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria ni hali inayoletwwa na ongezeko kubwa la bakteria waishio ndani ya uke hivyo kuwazidi bakteria walinzi ambao pia huishi ndani ya uke. Kupotea kwa uwiano wa bakteria hawa hupelekea kuonekana kwa dalili za vajinosisi ya bakteria.
Kuharibika kwa uwiano husababisha mwili kushambulia bakteria hao kwa kuamsha chembe ulinzi mbalimbali ukeni. Matokeo ya mpambano wa chembe ulinzi na bakteria hupelekea kutokea kwa michomo ya kinga za mwili ukeni na kuonekana kwa dalili mbalimbali zinazoashiria vajinosis ya bakteria.
Licha ya tatizo hili kuathiri sana wanawake walio kwenye umri wa uzazi, yaani miaka 15 hadi 45, linaweza kutokea kwenye umri wowote pia. Vihatarishi vya ugonjwa huu ni kuwa na mpenzi mpya au kushiriki ngono na wanaume wengi, kujisafisha uke sana na kemikali kali n.k.hata hivyo vajinosis ya bakteria si miongoni mwa magonjwa ya zinaa kwa sababu huwa hauambukizwi kwa ngono.
Matibabu ya vajinosisi ya bakteria yanapatikana na watu hutibiwa na kupona, hata hivyo tatizo linaweza kujirudia baada ya muda wa miezi kadhaa kupita.
Dalili
Wanawake wengi wenye ugonjwa wa vajinosis ya bakteria huwa hawaonyeshi dalili au ishara yoyote, hata hivyo endapo dalili zitatokea zinajumuisha;
Kutokwa na ute mwembamba, rangi ya kijivu au mweupe kama maziwa
Kutokwa na harufu mbaya ukeni mithiri ya harufu ya samaki haswa baada ya kujamiana
Hisia za kuungua, kuwashwa ukeni au maeneo yanayozunguka tundu la uke kwa nje
Maumivu wakati wa kukojoa( kuungua ukeni wakati wa kukojoa au majimaji yanapopita)
Visababishi
Visababishi vya vajinosisi ya bakteria ni kuzaliana kupita kiasi kwa bakteria waishio ukeni. Uke huwa na bakteria walinzi, na bakteria hawa hufaidika nao kwa kupatiwa chakula na makazi ukeni, bakteria hao huitwa lactobacillus. Mara nyingi idadi ya lactobacillus huwa kubwa kuliko bakteria wengine wanaoishi ukeni wenye jina la Gardnerella vaginalis.
Endapo bakteria Gardnerella vaginalis amepata upenyo wa kuzaliana, huzaliana kupita kiasi na kuzidi idadi ya bakteria lactobacillus na hivyo kuharibu uwiano wa bakteria hao. Uwiano unapoharibika, hupelekea kuamka kwa dalili za vajinosis ya bakteria.
Baadhi ya sababu zinazoweza pelekea kupungua kwa idadi ya bakteria walinzi yaani lactobacillus na hivyo kutoa upenyo wa kuzaliana kwa bakteria Gardnerella vaginalis ni kusafisha ndani ya uke na sabuni kali au au mara kwa mara n.k
Vihatarishi
Vihatarishi vinavyofahamika vinavyopelekea kupata tatizo la vajinosis ya bakteria ni;
Kuwa na wapenzi wengi au kushiriki ngono na mpenzi mpya
Kujisafisha ndani ya uke kwa kutumia sabuni au kemikali
Kuwa na uke usio au wenye idadi ndogo lactobacillus
Kusafisha nguo za ndani na sabuni au kemikali kali
Kujitosa mwili kwenye jakuzi(beseni) la maji yaliyotiwa viuaji vimelea wakati wa kuoga
Kutumia marashi ya kuweka ukeni
Kuvuta sigara
Matendo yasiyo hatarishi
Huwezi kupata ugonjwa wa vajinosis ya bakteria kwa;
Kuogelea kwenye bwawa
Kutumia choo cha kukaa
Kushika vitu
Kulala kitandani au kujifunika mashuka
Namna ya kujikinga na ugonjwa wa vajisosis ya bakteria
Acha kuwa na wapenzi wengi ili upunguze hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa
Tumia kondomu endapo unashiriki ngono na mpenzi mpya ili kuzuia kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa
Unapokuwa unasafisha uke, usitumie sabuni au visafisha uke kwa sababu uke una njia asili ya kijisafisha wenyewe. Tumia maji ya kawaida tu na epuka kujisafisha mara kwa mara bila sababu isipokuwa endapo umeshiriki ngono.
Usitumie pedi za kuchomeka zenye viua bakteria wa ukeni
Vipimo na uchunguzi wa vajinosis ya bakteria
Utakakuwa unaonwa na daktari, atakuuliza maswali mbalimbali kuhusu dalili na vihatarishi kisha atafanya uchunguzi wa uke na kuchukua sampuli ya majimaji ndani ya uke kwa ajili ya vipimo mbalimbali endapo vitahitajika ikiwa pamoja na kipimo cha PH.
Matibabu ya vajinosis ya bakteria
Matibabu ya vajinosis ya bakteria huhusisha matumizi ya dawa za antibayotiki zinazofahamika kutibu tatizo hili. Dawa zinazoweza kutumika ni za kumeza au kuchoma kwenye mishipa au kupaka ukeni.
Kusoma kuhusu dawa nenda kwenye makala ya ‘dawa za vajinosis ya bakteria’ ndani ya tovuti ya ulyclinic.
Matibabu ya pande mbili kwa wanaoshiriki ngono ya jinsia moja yanatakiwa?
Endapo unashiriki ngono ya jinsia moja yaani KE kwa KE, wote mnapaswa kupata matibabu kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi mapya kutoka kwake.
Endapo unashiriki ngono ya KE kwa ME, hakuna faida ya kumpatia matibabu ME kwa sababu ugonjwa huu huwa hauambukizwi kutokwa kwa mwanaume kwenda kwa mwanamke.
Je ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza kujirudia baada ya matibabu?
Ndio!
Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza kujirudia miezi michache hadi mwaka baada ya matibabu. Endapo tatizo litajirudia, utafanyiwa uchunguzi na kupewa dawa aina nyingine.
Tafiti hata hivyo zinaendelea kuangalia kama tiba ya kuongezewa bakteria wa lactobacillus inaweza kuwa suluhisho la kutibu vajinosis ya bakteria inayojirudia ndani ya muda mfupi.
Madhara ya vajinosis ya bakteria
Madhara yamegawanyika kwenye makundi mawili;
Madhara kwa mama mjamzito
Madhara kwa mjamzito na mwanamke asiye mjamzito
Madhara ya vajinosis ya bakteria kwa mama mjamzito
Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza leta madhara yafuatayo kwa mama mjamzito endapo matibabu hayatafanyika ipasavyo;
Kujifungua kabla ya muda hivyo kupata mtoto njiti
Kujifungua mtoto mwenye umri mdogo
Madhara ya vajinosis ya bakteria kwa mjamzito au asiye mjamzito
Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza leta madhara yafuatayo kwa wanawake endapo matibabu hayatafanyika ipasavyo;
Kupata magonjwa ya zinaa kama UKIMWI, kisonono, kaswende, herpes, chlamydia n.k
Kuambukiza mpenzi wako VVU endapo tayari una maambukizi
Hatari ya kupata maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji wa via vya uzazi au baada ya kusafishwa kizazi
Kupata ugonjwa wa PID
Ugumba endapo umepata tatizo la PID kwa muda mrefu bila matibabu
Wakati gani uonene na daktari haraka ukiwa na vajinosisi ya bakteria?
Onana na daktari endapo una ;
Tokwa na uchafu ukeni wenye harufu kali au kuwa na rangi isiyo ya kawaida au usio w akawaida kwako
Una wapenzi wengi na umepata mpenzi mpya na kwa sasa unapata dalili za magonjwa ya zinaa
Dalili zinaendelea licha ya kufanya juhudi binafsi za kujitibu mfano kutibu fangasi n.k
Mambo ya kutofanya ili kuepuka bacteria vaginosis
Usifaynye mambo yafuatayo ili kuepuka kupata bakteria vaginosis;
Kuoga muda mrefu kwa kujitosa kwenye beseni lenye maji ya moto
Kujitosa kwenye beseni lenye maji au sabuni kali kwa muda mrefu
Kujisafisha mara kwa mara ukeni au kujisafisha kupita kiasi
Kujisafisha kwa kutumia kemikali kali ndani ya uke
Kutumia mamukato ya kuweka ukeni
Majina mengine ya vajinosis ya bakteria huitwaje?
Baadhi ya majina mengine yanayoashiria vajinosis ya bakteria ni;
Bacteria vaginosis
Vaginal bacteriosis
Wapi utapata taarifa zaidi kuhusu Vaginosis ya bakteria?
Pata taarifazaidi kwenye makala za magonjwa zilizo ndani ya tivuti ya ULY CLINIC au kwa kutumia rejea ambazo zimeandikwa chini ya tovuti hii.