top of page

Mwandishi:

Dkt. Sospeter M, MD

Mhariri:

Dkt. Lugonda B, MD

Alhamisi, 15 Julai 2021

Kufunga uzazi -Mwanamke

Kufunga uzazi -Mwanamke
Kufunga uzazi -Mwanamke
Kufunga uzazi -Mwanamke

Kufunga uzazi kwa mwanamke hufahamika kwa jina jingine la kufunga mirija ya uzazi au kufunga kizazi ni njia mojawapo ya uzazi wa mpango inayochaguliwa na wanawake wasio na uhitaji tena wa kupata watoto. Njia hii huwa na uwezo wa kuzuia kupata mimba kwa asilimia 100. Katika makala hii neno kufunga uzazi na kufunga mirija ya uzazi imetumika kumaanisha kufunga uzazi kwa kukata mirija ya uzazi.


Kuna aina mbalimbali za upasuaji wa kufunga mirija ya kufunga uzazi, ikiwa pamoja na upasuaji wa kuanzisha makovu ndani ya mirija ya uzazi, upasuaji wa kubana mirija ya uzazi au upasuaji wa kuachanisha mirija ya uzazi.


Mbali na aina hizi za upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi, upasuaji huo unaweza kufanikishwa kwa njia kuu mbili kwa sasa, yaani nnjia ya kutumia laparaskopi (au upasuaji wa kilaparaskopiki) au njia ya kutoboa sehemu ndogo ya tumbo ili kufikia mirija ya uzazi na ovari.


Kila njia ya kufunga mirija ya uzazi ina faida na hasara zake, aina nzuri ya njia unayopaswa kuchagua ni ile itakayokupa uwezekano wa kufungua uzazi pale itakapotokea umebadili mawazo ya kuzaa tena baada upasuaji.


Wakati gani sahihi wa kufanya upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi?

Unaweza kufanyiwa upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi muda wowote ule kama;

  • Wakati wa kujifungua kwa njia ya uke

  • Wakati wa kujifungua kwa upasuaji

  • Wakati wa upasuaji mwingine wa tumbo

  • Wakati wowote baada ya kujifungua


Kufunga uzazi wakati wa upasuaji wa kujifungua hushauriwa zaidi na wataalamu kwa kuwa huzuia athari za kufanyiwa upasuaji mwingi zaidi unaoweza kukupelekea kpata makovu ndani ya matumbo


Madhumuni ya kufunga mirija ya uzazi

Kufunga mirija ya uzazi hufanyika kama njia mojawapo ya kudumu ya uzazi wa mpango kwa wanawake. Njia hii huzuia daima uwezo wa mwanamke kubeba mimba na humfanya mwanamke asihitajikutumia njia zingine za uzazi wa mpango kama vidonge na sindano au vizuizi au kutumia kondomu n.k.


Je kufunga uzazi kunazuia kupata magonjwa ya zinaa?


Hapana! kufunga uzazi hakuzuii kupata magonjwa ya zinaa isipokuwa huzuia kupata ujauzito tu, endelea kumia kondomu ili kujikinga na magonjwa ya zinaa au kuacha kushiriki ngono kabisa ili kujikinga.


Faida za kufunga uzazi

Faida ya kwanza ya kufunga uzazi kwa kufunga mirija ya uzazi ni kuzuia uwezekano wa kupata ujauzito kwa asilimia 100. Faida zingine ni kuzuia uwezekano wa kupata saratani ya ovari kwa wanawake.


Hasara za kufunga uzazi

Upasuaji wa kufunga uzazi haufanyiki kwa kila mwanamke. Utashauriwa na mtaalamu wa afya kuhusu faida, madhara na hatari ya kufunga uzazi na kupewa uchaguzi wa njia nyingine zinazoweza kuzuia ujauzito kwa ufanisi kabla ya kufanayiwa upasuaji huu.


Madhara ya upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi

Upasuaji wa kufunga uzazi huwa na madhara yanayofanana na upasuaji mwingine wa tumboni na baadhi ya madhara ni ya moja kwa moja. Madhara yanaweza kuwa:


  • Kuvia damu ndani ya tumbo

  • Kupata maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji

  • Kufumuka kwa kidonda cha upasuaji

  • Uharibifu wa kibofu cha mkojo, mirija ya mkojo na mishipa mikuu ya damu tumboni

  • Kovu kwenye eneo lililofanyiwa upasuaji au makovu ndani ya tumbo

  • Maumivu endelevu ya tumbo kutokana na makovu ndani ya tumbo

  • Kupata ujauzito endapo upasuaji haukuwa wa mafanikio au mirija imejiunga


Mambo yanayoongeza hatari ya kupata madhara ya upasuaji wa kufunga uzazi



Mambo yafuatayo yanaongeza hatari ya kupata madhara ya upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi;


  • Kuwa na historia ya upasuaji mwingine wa tumbo

  • Kuwa na uwiano wa uzito mkubwa au ugonjwa wa obeziti

  • Kuwa na ugonjwa wa kisukari

Nini unatakiwa kufahamu kabla ya upasuaji wa kufunga uzazi?

Kabla ya kufanyiwa upasuaji wa kufunga uzazi, unatakiwa kufahamu mambo yatakayoweza kukufanya ubadili mawazo ya kufanya upasuaji huo au yatakayokufanya ujutie hapo baadae. Mambo yanayoweza kukufanya ujutie au kubadili mawazo ni;


  • Kuwa na mpenzi mpya ambaye anahitaji kuwa na watoto nawe

  • Kuwa na umri mdogo chini ya miaka 35, umri mdogo unakupa uwezekano wa kupata mpenzi mpya anayehitaji watoto

  • Kuachika na mwanaume uliyenaye baada ya kupoteza uwezo wa kupata watoto

  • Uwezekano wa kutopata tena mtoto na kuferi kwa upasuaji wa kufungua uzazi


Naweza kwenda nyumbani siku hiyo baada ya kufanyiwa upasuaji wa kufunga uzazi?

Ndio, mara nyingi baada tu ya upasuaji wa kufunga uzazi hufanyika unaweza kuruhusiwa kwenda nyumbani siku hiyo au siku inayofuata. Hata hivyo unaweza kulazwa endapo utahitaji kufanyiwa uangalizi wa karibu baada ya kufanyiwa upasuaji.


Kabla ya upasuaji nini hufanyika?

Kabla ya kufanyiwa upasuaji wowote, lazima vipimo mbalimbali vya damu vifanyike ili kuangalia kama inafaa kwako kufanyiwa upasuaji au la ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea. Vipimo vinaweza kufanyika miongoni mwake ni;

  • Kipimo cha picha halisi ya damu ( kuangalia wingi wa damu n.k)

  • Kipimo cha kuangalia uwezo wa damu kuganda

  • Kipimo cha ujauzito kwa njia ya mkojo

  • Vipimo vingine kama Picha mionzi sauti ya tumbo n.k


Naweza kufunga uzazi nikiwa mjamzito?

Hapana huwezi kufunga uzazi endapo una ujauzito, utasubiria hadi wakati wa kujifungua ndipo ufunge uzazi.


Namna upasuaji wa kufunga uzazi unavyofanyika

Kuna aina mbalimbali za upasuaji wa kufunga uzazi ambazo ni;


  • Upasuaji wa laparaskopiki

  • Upasuaji wa kuchana sehemu ndogo ya tumbo


Upasuaji wa laparaskopiki

Hufanyika kwa kutoboa tundu dogo kwenye kuta za tumbo kisha kuingiza laparaskopi kupitia tundu hilo. Kifaa hiki huongozwa na daktari ili kiweze kutengenisha mirija ya uzazi kwa kuiharibu, kuikata na kisha kuifunga kwa nyuzi au kuibana kwa kibanio maalumu.


Upasuaji wa kuchana sehemu ndogo ya tumbo

Upasuaji huu hufanyika kwa kuchana sehemu ndogo pembeni ya kitovu ili kuweza kuifikia mirija ya uzazi kisha kuitengenisha kwa kuikata na kuishona. Baada ya kutengenishwa mirija hii ya uzazi hufungwa fundo ili isiweze kujiunganisha.


Baada ya upasuaji utegemee nini?

Baada ya kufanyiwa upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi utapata maudhi madogo ya upasuaji kama vile;

  • Maumivu ya tumbo

  • Uchovu

  • Kizunguzungu

  • Tumbo kujaa gesi

  • Maumivu ya bega


Utapatiwa dawa za maumivu kabla ya kwenda nyumbani, mara nyingi baada ya masaa 48. Unaweza elekezwa kurejea hospitali kwa uchunguzi baada ya muda Fulani kupita.


Baada ya kwenda nyumbani unapaswa kuzingatia utunzaji wa kidonda cha upasuaji kwa kuzuia mvutano mkubwa au kutia maji kama ulivyoshauriwa na daktari wako. Kwa maelezo zaidi ya namna ya kutunza kidonda cha upasuaji ingia kwenye Makala ya ‘kutunza kidonda cha upasuaji’ sehemu nyingine kwenye tovuti hii ya ulyclinic.


Ufanisi wa upasuaji wa kufunga kizazi

Tafiti zinaonyesha upasuaji wa kufunga uzazi huwa na ufanisi wa asilimia 99, yaani ni mwanamke mmoja tu kati ya wanawake 100 waliofunga kizazi anaweza kupata ujauzito ndani ya mwaka mmoja baada ya kufunga mirija ya uzazi. Kupata ujauzito baada ya upasuaji huu hutegemea umri wako, jinsi unavyokuwa na umri mdogo, uwezekano wa kupata ujauzito huongezeka na haswa ujauzito wa nje ya mfuko wa kizazi.


Je inawezekana kufungua mirija ya uzazi baada ya kufungwa?

Baada ya kufunga mirija ya uzazi, mara nyingi ni vigumu kuifungua na kupata mtoto kama ilivyokuwa awali. Hata hivyo upasuaji wa kufungua uzazi unaweza kufanyika licha ya matokeo kutokuwa ya kuridhisha.


Daktari atakufanyia uchunguzi kuona kama inafaa kufungua mirija ya uzazi na kupata matokeo chanya ya kubeba ujauzito au utumie njia zingine. Kwa maelezo zaidi kuhusu mambo gani yanaweza kumwambia daktari amue kufanya upasuaji au la, ingia kwenye Makala ya ‘kufungua uzazi’ sehemu nyingine katika tovuti hii ya ULY CLINIC.


Ruksa na mwiko baada ya kufanyiwa upasuaji wa kufunga uzazi

Usifanye mambo yafuatayo baada ya upasuaji wa kufunga kizazi ili kuepuka kupasuka kwa kidonda au kutofunga vema;

  • Kunyanyua vitu vizito ndani ya miezi mitatu

  • Kujamiaa ndani ya kipindi ambacho umekatazwa kufanya hivyo


Naweza kufanya kazi zangu baada ya upasuaji wa kufunga kizazi?

Ndio unaweza kurejea taratibu kufanya kazi zako za kila siku baada ya upasuaji wa kufunga kizazi, hakikisha hufanyi kazi nzito zenye mgandamizo mkubwa kwenye kidonda ili kuepuka kidonda chako kutengana au kuchelewa pona.


Wakati gani uwasiliane na daktari haraka baada ya upasuaji wa kufunga uzazi?

Wasiliana na daktari wako mara moja endapo una dalili zifuatazo;


  • Joto la mwili linapanda kufika zaidi ya nyuzijoto za sentigredi 38

  • Kuzimia au kupoteza fahamu

  • Maumivu makali ya tumbo yanayoongezeka baada ya masaa 12 toka umefanyiwa upasuaji

  • Kutokwa na damu kwenye kidonda au gozi iliyofunika kidonda kulowa damu

  • Kutokwa na uchafu unaonuka kwenye kidonda

ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia linki ya 'mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii au kwa kubofya 'pata tiba'

Imeboreshwa,

21 Januari 2023, 16:54:54

Rejea za mada hii;

1. Hatcher RA, et al. Female Sterilization: Tubal Ligation or Occlusion. In: Managing Contraception 2017-2018. 14th ed. Tiger, Georgia: Bridging the Gap Foundation.http://www.acog.org/Patients/FAQs/Sterilization-by-Laparoscopy. Imechukuliwa 15.07.2021

2. Sarah Marino, et al.Tubal Sterilization. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK470377/. Imechukuliwa 15.07.2021

3. ACOG Practice Bulletin No. 208 Summary: Benefits and Risks of Sterilization. Obstet Gynecol. 2019 Mar;133(3):592-594.

4. Danis RB, et al. Postpartum Permanent Sterilization: Could Bilateral Salpingectomy Replace Bilateral Tubal Ligation? J Minim Invasive Gynecol. 2016 Sep-Oct;23(6):928-32.

5. Castellano T, et al. Risks and Benefits of Salpingectomy at the Time of Sterilization. Obstet Gynecol Surv. 2017 Nov;72(11):663-668. [PubMed]

6. Zerden ML, et al. Risk-Reducing Salpingectomy Versus Standard Tubal Sterilization: Lessons From Offering Women Options for Interval Sterilization. South Med J. 2018 Mar;111(3):173-177.

7. Kim AJ, et al. The Trend, Feasibility, and Safety of Salpingectomy as a form of Permanent Sterilization. J Minim Invasive Gynecol. 2019 Nov - Dec;26(7):1363-1368.

8. Ludermir AB, et al. Tubal ligation regret and related risk factors: findings from a case-control study in Pernambuco State, Brazil. Cad Saude Publica. 2009 Jun;25(6):1361-8.

9. Timothy C. Rowe, et al. Female Tubal Sterilization
https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2327446/. Imechukuliwa 15.07.2021

10. Shilpa Vishwas Date, et al. Female sterilization failure: Review over a decade and its clinicopathological correlation. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4137647/. Imechukuliwa 15.07.2021

bottom of page