Mwandishi:
Dkt. Salome A, MD
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
Alhamisi, 15 Julai 2021
Kufunga uzazi- Mwanaume
Kufunga uzazi kwa mwanaume hufahamika kwa jina jingine la vasektomi, ni mojawapo ya njia ya uzazi wa mpango wa kudumu kwa mwanaume. Njia hii hufanyika kwa kukata mrija wa vas diferensi unaobeba mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ili kuzifikisha kwenye mrija wa mkojo uitwao yurethra na kuzitoa nje wakati wa kufika kileleni. Upasuaji wa kufunga uzazi kwa mwanaume unaweza kufanywa kwa ganzi tu bila kutumia dawa za kaputi na baada ya upasuaji, mara nyingi mgonjwa huenda nyumbani siku hiyo hiyo. Kabla ya kufanyiwa upasuaji huu ni lazima kutafakari kuhusu athari za baadae za maamuzi magumu unayoyotaka kufanya. Ni vema kuwa na uhakika kuwa huhitaji mtoto hapo baadae, hii ni kwa sababu licha ya kuwea kufanyiwa upasuaji wa kufungua uzazi, ufanisi wa matibabu hayo huweza kuwa mdogo kwa baadhi ya watu.
Je kufunga uzazi hukinga maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwa mwanaume?
Hapana! Kufunga uzazi hakuzuii kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama klamidia, kisonono, kaswende VVU n.k. Utahitajika kutumia njia za kujikinga na magonjwa ya zinaa mfano kuvaa kondomu, kutoshiriki ngono au kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu asiye na magonjwa ya zinaa.
Madhumuni ya kufunga uzazu kwa mwanaume
Kufunga uzazi ni njia mojawapo ya uzazi wa mpango yenye ufanisi mkubwa na ya kudumu. Njia hii huchaguliwa na wanaume wenye uhakika kuwa hawahitaji watoto sasa na hapo baadae.
Faida za kutumia uzazi wa mpango kwa kufunga uzazi kwa mwanaume
Njia hii ina ufanisi wa asilimia 100 kuzuia ujauzito
Huweza kufanyika kirahisi na kuondoka bila kulazwa
Huwa na maudhi kidogo baada ya upasuaji
Ni ya gharama kidogo ukilinganisha na kufunga uzazi wa mwanamke au kutumia dawa za uzazi wa mpango kwa mwanamke
Huondoa haja ya kutumia njia za uzazi wa mpango kwa mwanamke kama kondomu au dawa za uzazi wa mpango
Maudhi na madhara ya kufunga uzazi kwa mwanaume
Madhara ya upasuaji wa kufunga uzazi kwa mwanaume ni kutopata mtoto kabisa na kupunguza uwezekano huo licha ya hapo baadae kufanyiwa upasuaji wa kufungua uzazi.
Maudhi ya muda mfupi ya upasuaji wa kufunga uzazi ni;
Kutokwa damu au kuganda kwa damu ndani ya korodani
Kutoa shahawa zenye damu
Korodani kuvilia damu
Maambukizi kwenye mshono wa upasuaji
Maumivu ya korodani
Kuvimba kwa korodani
Maudhi ya baadaye ya kufunga uzazi ni;
Maumivu sugu kutokana na makovu ndani ya korodani
Korodani kujaa maji
Maumivu wakati wa kufika kileleni
Michomo kwenye korodani kutokana na kuvia kwa mbegu za kiume kwenye korodani
Kutungisha ujauzito endapo upasuaji haukufanikiwa vema
Kutungishwa kwa vifuko vya maji kwenye mrija wa epididimiz
Kupata busha ( kuvimba kwa korodani)
Je kufunga uzazi kwa mwanaume hupunguza nguvu za kiume?
Hapana! Kufunga uzazi kwa mwanaume hakuwezi punguza nguvu za kiume wala hamu ya maoenzi au kuathiri misuli au afya yako kwa ujumla isipokuwa itakufanya usiwe na uwezo wakubebesha mimba tu.
Je kufunga uzazi hupelekea uharibifu wa via vya uzazi wa mwanaume?
Ndio! Kuna uwezekano mdogo sana wa kujeruhiwa kwa korodani, uume na via vingine vya uzazi wakati wa kufanyiwa upasuaji. Kama upasuaji utaathiri mishipa ya damu ya korodani, hupelekea kupoteza korodani lakini hutokea kwa nadra sana na mara nyingi kama umefanyiwa upasuaji na mtu asiye mzoefu na upasuaji huu.
Je kufunga uzazi huongeza hatari ya kupata saratani kwa mwanaume?
Hakuna ushahidi wa tafiti kuthibitisha uvumi huu wa kitambo kwamba kufunga uzazi kwa mwanaume ni kihatarishi cha saratani ya tezi dume au korodani.
Je kufunga uzazi kunaongeza hatari ya magonjwa ya moyo kwa mwanaume?
Hakuna ushahidi mpaka sasa wa tafiti unaohusianisha kufunga uzazi na magonjwa ya moyo kama inavyohofiwa na watu wengi toka zamani.
Je kufunga uzazi husababisha maumivu ya muda mrefu ya korodani?
Unaweza kupata maumivu ya wastani au hisia za kuvuta ndani ya korodani kisha hupotea siku zinavyokwenda kwa wanaume wengi. Baadhi ya wanaume wanaweza kupata maumivu ya muda mrefu kama kumefanyika makovu mengi ndani ya korodani
Maandalizi ya kufanya kabla ya upasuaji wa kufunga uzazi
Fanya maandalizi yafuatayo kabla ya kufanyiwa upasuaji;
Usitumie dawa za kuyeyusha damu siku chache kabla ya upasuaji ili kuepuka hatari ya kutokwa na damu nyingi wakati au baada ya upasuaji
Nunua nguo za ndani za kubana ziwezeshe kubeba vema korodani na kuzifanya zisicheze wakati unatembea baada ya kufanyiwa upasuaji
Oga na safisha meneo ya siri kwenye uume na korodani pamoja na kunyoa mavuzi kabla ya upasuaji
Andaa usafiri kukufikisha nyumbani kwako baada ya upasuaji. Usafiri mzuri ni ule ambao hauna mtikisiko mkubwa wa mwili wako na hausababishi kutonesha kidonda cha upasuaji.
Jinsi gani upasuaji wa kufunga uzazi unafanyika?
Upasuaji wa kufunga uzazi kwa mwanaume huweza fanyika katika ofisi ya daktari siku ambayo umepanga kuonana naye. Utachomwa sindano ya ganzi eneo linalofanyiwa upasuaji kisha kufanyiwa upasuaji huo kwa muda wa dakika 10 hadi 30. Upasuaji huu huwa na hatua zifuatazo;
Kuchoma ganzi kwenye eneo linalochanwa kwa kutumia sindano
Kuchana mchano mdogo kwenye ngozi sehemu ya juu ya korodani kwa kutumia kisu kisha kuchokonoa na vidole ili kuweza kufikia mrija wa vas diferensi
Kutafuta mrija wa vas deferens ulipo kwa kutokea kwneye korodani
Kuvuta nje mrija wa vas deferens kicha kukata kwenye vipande viwili
Kufunga vipande vya mirija wa vas diferensi iliyokatwa kwa kuichoma, kufunga na uzi au kuweka vibanio
Kurejesha miishio ya mrija wa vas diferensi iliyofungwa ndani ya mwili
Kufunga kwa kidonda kwa nyuzi au gundi
Utegemee nini baada tu ya kufanyiwa upasuaji wa kufunga kizazi?
Baada ya upasuaji wa kufunga kizazi, tegemea kupata maumivu, kuvilia damu, na kuvimba kwenye maeneo ya pumbu au korodani. Dalili hizi zitapotea kwa jinsi siku zinavyokwenda, mara nyingi huchukua wiki moja hadi mbili kisha kuisha.
Dalili gani zikufanye uwasiliane haraka na daktari baada ya upasuaji wa kufunga kizazi?
Wasiliana na daktari wako haraka endapo una dalili zifuatazo;
Dalili za maambukizi kwenye korodani au kidonda cha upasuaji kama vile kutokwa na damu, kupanda kwa joto la la kidonda, maumivu yanayoongezeka na kuongezeka kwa mvio wa damu.
Kupata homa au joto la mwili kuzidi nyuzi joto za sentigredi 38
Nini cha kufanya nyumbani baada ya upasuaji wa kufunga uzazi?
Hakikisha unafanya mambo yafuatayo kukusaidia kupona haraka kwa jinsi utakavyoshauriwa na daktari wako; Saidia korodani zako zisicheze cheze kwa kuvaa nguo ya ndani inayobana korodani kwa angalau masaa 48 baada ya upasuaji. Hii itasaidia kuacha kutonesha kidonda na kuzuia kutokwa na damu pia kuongeza kasi ya kupona Kanda kwa kutumia barafu iliyofingwa vema kwenye nailoni eneo la korodani lililofanyiwa upasuaji siku mbili za mwanzo baada ya kufnayiwa upasuaji. Usifanye kazi nzito baada ya upasuaji, pumzika angalau kwa muda wa masaa 24 kisha unaweza kufanya kazi ndogondogo baada ya siku tatu hadi nne na kuongeza jinsi siku zinavyokwenda na jinsi maumivu yanavyoisha.
Usishiriki ngono kwa muda wa wiki moja au zaidi kwa sababu utahisi maumivu. Hata hivyo unaweza kupata shahawa zenye damu baada ya kupona na hili litaisha lenyewe.
Je unaweza kufanya mapenzi bila kinga wiki chache baada ya upasuaji na kutotungisha mimba?
Hapana! Unatakiwa kutumia kinga au njia zingine za uzazi wa mpango mpaka pale daktari wako atakapothibitisha kuwa hakuna mbegu za kiume kwenye shahawa zako.hili litafanyika kwa kupima uwepo wa manii kwenye shahawa
Ufanisi wa upasuaji wa kufunga kizazi kwa mwanaume
Baada tu ya kufanyiwa upasuaji, baadhi ya mbegu za kiume zilizobaki kwenye mirija ya uzazi zinawez akuwa chanzo cha kutungisha ujauzito. Hii ndio maana utatakiwa kukaa kwa miezi kadhaa na kumwaga shahawa angalau mara 15 hadi 20 mpaka pale shahawa zitakapoisha kabisa. Wakati huu unashauriwa kutumia njia zingine za uzazi wa mpango mpaka itakapothibitishwa kuwa hakuna mbegu za kiume kwenye shahawa zako. Baada ya kuthibitishwa kuwa hakuna mbegu za kiume wkenye shahawa, utaweza kujamiana bila kutumia kinga na ujauzito utazuiwa kwa asilimia 100.
Kuna njia zingine za kuweza kupata mtoto baada ya kufunga uzazi?
Ndio!
Kuna njia zingine unazoweza kutumia kutoa mbegu za kiume kutoka kwenye korodani kisha kuchavusha yai kwenye chupa ya uzazi kabla ya kupandikizwa kwenye kizazi cha mpenzi wako. Njia hii huwa na gharama pia huhitaji utaalamu mkubwa, hivyo kabla ya kufunga uzazi unatakiwa kufikiria mara mbili kabla ya kufanya hivyo.
ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia linki ya 'mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii au kwa kubofya 'pata tiba'
Imeboreshwa,
21 Januari 2023, 16:54:39
Rejea za mada hii;
1. American Urological Association . Vasectomy. https://www.auanet.org/guidelines/vasectomy-(2012-reviewed-for-currency-2015). Imechukuliwa 15.06.2021
2. Armand Zini, MD, et al. CUA guideline: Vasectomy. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5110415/. Imechukuliwa 15.07.2021
3. Dane Johnson, et al. Vasectomy: tips and tricks. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5583057/. Imechukuliwa 15.07.2021
4. Duan H, et al. Association between vasectomy and risk of testicular cancer: A systematic review and meta-analysis. PLoS One. 2018;13:e0194606.
5. Gavin Stormont, et al. Vasectomy. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK549904/. Imechukuliwa 15.07.2021
6. P J Schwingl, et al. Safety and effectiveness of vasectomy. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/10785217/. Imechukuliwa 15.07.2021
7. Ranjith Ramasamy, e tal. Vasectomy and vasectomy reversal: An update. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3114592/. Imechukuliwa 15.07.2021
8. Taneja SS, et al., eds. Complications of surgery of the testicle, vas deferens, epididymis, and scrotom. In: Taneja's Complications of Urologic Surgery: Diagnosis, Prevention, and Management. 5th edition. Edinburgh, U.K.: Elsevier; 2018. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 15.06.2021
9. Urology Care Foundation. What is a vasectomy?. https://www.urologyhealth.org/urologic-conditions/vasectomy/printable-version. Imechukuliwa 15.06.2021
10. Urology Care Foundation. Vasectomy. https://www.urologyhealth.org/educational-materials/vasectomy. Imechukuliwa 15.06.2021
11. Vasectomy. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 15.06.2021