Mwandishi:
ULY CLINIC
30 Aprili 2020, 10:52:23
Mambo yanayo kwamisha mazoezi
Wakati wa pilika za leba na kujifungua, unategemewa kuwa mtulivu, kupumua kawaida, kujishughulisha na kufuata maelekezo unayopewa, hata hivyo utaambiwa kukaa pozi tofauti tofauti. Hii ni muhimu sana wakati huu kwa afya yako na mtoto tumboni. Kama umezoea kufanya mazoezi yenye mpangilio maalumu kama vile kuogelea, kutembea, kuendesha baiskeli, hakuna sababu ya kwanini usiendelee na mazoezi hayo. Kama unaishi kijijini pia, endapo ulikuwa unajishughulisha na shughuli za kutoa jasho mfano kufua, kulima, kuosha vyomba kuchota maji, kuendesha baiskeli n.k hauna sababu ya kusimamisha kazi hizo mara unapopata mimba isipokuwa endapo hujihisi vema kiafya au mazoezi yamekuwa mazito kuliko uwezo wako.
Kipindi cha ujauzito si kipindi cha kuanza kufanya mazoezi mapya makali mfano kuruka viunzi, na mengineyo, hata hivyo utatakiwa kuwa na vipindi vya kupumzisha mwili wako kila siku.
Wakati mwingine mazoezi wakati wa ujauzito yanaweza kuwa ya hatari kwa mama mtarajiwa au kwa mtoto au wote wawili. Mjamzito yeyote anapotaka kuanza kufanya mazoezi ni lazima kwanza apate ushauri kutoka kwa daktari/mkunga. Magonjwa na hali ambazo zinatakiwa kupewa umakini na zinazozuia mazoezi kufanyika kwa ufanisi ni;
Mimba iliyotishia kutoka/abosheni
Maumivu ya maungio ya mwili
Ujauzito mapacha
Magonjwa ya moyo
Maumivu makali nyuma ya mgongo
Shinikizo la juu la damu kutokana na ujauzito
Inashauri kutofanya mazoezi ya kuchuchumaa endapo mwanao tumboni bado amelala sambamba na mwili wako na kutanguliza matako chini. Kufanya mazoezi ya kuchuchumaa humfanya mtoto akae kwenye pozi hilohilo na kutogeuka kwa ajili ya kutanguliza kichwa. Hata hivyo mara unapotambua kwamba mwanao amelala kwa kutanguliza kichwa chini, fanya mazoezi ya kuchuchumaa mara nyingi uwezavyo jinsi unavyojihisi vema. Hii itasaidia kichwa cha mtoto kujongea chini zaidi kwenye tundu la uzazi na kusababisha mtoto asigeuke na usijifungue mtoto aliyetanguliza matako. Unapokwenda kliniki ya ujauzito hakikisha unamuuliza nesi au daktari kuhusu mwanao amelalaje tumboni.
Mtu yeyote mjamzito anaweza kufanya mazoezi, hata kama una mtindio wa ubongo au ni mtu wa makamo. Wanawake wajawazito wanaofanya mazoezi ya ratiba maalumu mara tatu kwa wiki huwa na leba na uzazi rahisi. Hata hivyo wakati wa ujauzito unatakiwa kuwa na mafunzo ya ziada kwa sababu hapa umebeba kiumbe na unafanya kazi ya ziada. Hutaweza kufanya vitu ambavyo ulikuwa unavifanya wakati hauna ujauzito, na hii inamaanisha unatakiwa kuhakikisha unafanya mazoezi kwa kiwango kinachotakiwa kiafya na kuyafanya yawe ya kawaida. Unaweza kutembea kilomita tatu na ukahisi umetembea kilomita sita, hii ni kawaida, hakikisha tu unauwezo wa kuongea kama kawaida na kuchukua tahadhari za usalama wako wakati unafanya mazoezi.
Wakati wa mazoezi damu nyingi huelekea kwenye ngozi na misuli, damu kiasi kidogo huingia kwenye ogani mbalimbali ndani ya mwili kama vile figo na ini. Kwa vile mjamzito anafanya kazi kubwa hata kama amekaa, ni vema kuacha kujitumikisha zaidi ya uwezo wako pia pata muda wa kupumzika wakati wa mchana na kulala.
Kama ukitaka kufanya mazoezi, wakati mzuri wa kufanya mazoezi hayo ni asubuhi kabla ya jua kuchomoza na jioni ambapo jua linapozama. Haishauriwi kupandisha joto la mwili sana kutokana na mazoezi, hivyo ndo maana muda huu wa asubuhi na jioni ni mzuri kwani hakuna jua kali. Kupanda kwa joto kupita kiasi kwa kipindi cha miezi miwili ya kwanza ya ujauzito ni kihatarishi cha kupata mtoto mwenye madhaifu ya kiuumbaji.
Endapo joto litazidi Zaidi kipindi cha kuanzia miezi minne na kuendelea, mama ana hatari ya kujifungua kabla ya wakati kufika. Unatakiwa kufahamu kwamba joto la mtoto tumboni huwa kubwa kuliko la mama, joto la mama linapoongezeka Zaidi ya mtoto tumboni husababisha mwili wa mtoto kushindwa kurekebisha joto lake kuwa katika kiwango kinachotakiwa kwa ajili ya ukuaji. Kama mwili wako utakuwa wa moto Zaidi wakati wa mazoezi, hakikisha unachukua hatua za kupunguza joto mazoezi yanayofuata kwa kufanya mazoezi wakati wa asubuh na mapema au jua linapozama, kuvaa nguo nyepesi Zaidi, kunywa maji ya kutosha, kufanya mazoezi kwa muda mfupi na usifanye mazoezi makali. Zuia mazoezi ya kuushinikiza mwili Zaidi wakati wa ujauzito kama vile mazoezi ya sauna. Licha ya kupaswa kuwa makini kwa kufuata kanuni za usalama wakati wa mazoezi, mazoezi bado ni ya umuhimu kukufanya uwe imara na upate wepesi katika ujauzito, leba na kujifungua.
Dalili zitakazokufanya usiendelee na mazoezi kwenye ujauzito
Mambo ambayo yatakulazimisha kusimamisha mazoezi ni
Kutokwa na damu ukeni
Kutokwa na maji mengi ukeni
Kuhisi kichwa chepesi au kuzimia
Kuishiwa pumzi
Kizunguzungu au kuhisi kichefuchefu
Wakati mwingine kizunguzungu kinaweza kusababishwa na njaa mfano mfungo, kutopata chakula bora na cha kutosha. Hakikisha kuwa unapata mlo kamili.
Vyakula wakati wa ujauzito
Orodha ya vyakula unavyoweza kuchagua kutengeneza mlo wako ni
Aina ya chakula
Vyakula vya protini
Mfano
Protini daraja la kwanza- Nyama, samaki, mayai, maziwa na maziwa mgando
Protini dawaja la pili- karanga, maharagwe na mimea jamii ya kunde mfano mbaazi
Vyakula vya wanga
Mfano ni mchele, viazi vitamu, mihogo, mkate, mtama, uwele n.k
Vyakula vyenye madini muhimu ya foliki asidikwa ajili ya uumbaji mzuri wa ubongo na uti wa mgongo
Mfano mboga za majani zenye rangi ya kijani na matunda
Kumbuka unahitaji kula matunda kwa wingi.
Soma Zaidi kuhusu makundi ya chakula kwenye tovuti hii kujua makondu yote ya chakula na umuhimu wake.
Kwa baadhi ya nchi na makabila wanakataza wanawake kula aina Fulani ya vyakula kama vile, mayai, nyama ya nguruwe n.k. Tamaduni hizi ni za hatari kwani wakati wa ujauzito mwili unahitaji virutubisho kwa wingi kuwezesha utengenezaji na ukuaji wa mtoto tumboni. Hata hivyo licha ya kuwa na umuhimu wa kupata virutubisho vya kutosha, kuongezeka uzito kupita kiasi ni hatari kiafya katika kipindi hiki. Hutakiwi ongezeka Zaidi ya kilo 11.5 katika kipindi kizima cha ujauzito, kati ya wiki 28 hadi 30 za ujauzito hutakiwi ongezeka Zaidi ya kilo 3.3 haswa kwa wale wenye mimba ya kwanza.
Kupata mlo kamili uliopangiliwa kutakuzuia kuongezeka uzito kupita kiasi na kuepuka hatari ya kujifungua mtoto njiti, kuongezeka kwa shinikizo lako la damu(presha) la mama na kuvimba. Hii ndio maana unahitajika kupimwa uzito kwa mpangilio. Vegetariani(wanaotumia vyakula vya mimea tu) wanatakiwa kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa lishe ili kuhakikisha kwamba kiwango cha chakula wanachokula kinakidhi mahitaji ya mama na mtoto aliye tumboni.
Umuhimu wa mazoezi wakati wa ujauzito
Mjumuisho kwa ufupi wa umuhimu wa mazoezi wakati wa ujauzito
Huimarisha mzunguko wa damu mwili mzima kwa kuongeza uwezo wa moyo kusukuma damu
Huongeze ufanisi wa moyo kusukuma damu mwilini na kumwondoa mama kwenye hatari ya kupata mshituko wa moyo
Huongeza ufanisi wa mapafu na kufanya hewa safi ya oksjeni iwepo kwa mama na mtoto
Hudhibiti ongezeko la Mafuta na uzito kupita kiasi kwa kuwa mwili hutumia Mafuta ya ziada
Huongeze mzunguko wa damu kwenye misuli na mifupa na hivyo huimarisha mifupa na kuipa nguvu na kufanya iwe fanisi Zaidi.
Faida za mazoezi kwa mtoto
Faida za mazoezi kwa mtoto
Huimarisha mahusiano ya mama na mtoto tumboni
Huchangamsha mtoto tumboni (mtoto tumboni hufurahia mijongeo ya mama na muziki unaopigwa)
Mama mwenye furaha na utulivu huwa na mtoto mwenye furaha na utulivu pia
Inasemekana kwamba, kipindi mtoto anapozaliwa, huwa ameshatengeneza mahusiano na mama yake toka akiwa tumboni. Wote hufurahia nyakati nzuri na za huzuni. Mtoto aliyetumboni husikiza sauti zinazotoka ndani na nje ya tumbo. Mtoto anapochangamshwa na sauti zozote zile akiwa tumboni mfano sauti ya mziki katika kipindi cha kuanzia miezi mitano anakuwa na uwezo wa kuitikia sauti alizo na uzoefu nazo. Mtoto akiwa tumboni na ameamka, huweza kuitikia sauti kwa kurusha miguu au kubadili pozi. Mimba inapofikisha umri wa miezi nane, mfumo wa usikivu huwa umeshakamilika kutengenezwa na mtoto anaweza kusikia vema sauti za mziki na watu.
Muulize daktari wako siku zote endapo mazoezi haya yatakufaa kulingana na hali ya afya yako.
ULY clinic inakukaribisha kwa ushauri na Tiba. Wasiliana nasi kupitia namba za simu au bonyeza kitufe cha ‘Pata Tiba’ chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
1 Oktoba 2021
American Pregnancy Association. Sleeping positions during pregnancy. Imechukuliwa 28.04.2020
National Sleep Foundation. The best position for sleep during pregnancy.Imechukuliwa 28.04.2020
National Posture Institute. Incorporating NPI’s 4 points of posture during pregnancy and postpartum. Imechukuliwa 28.04.2020
https://www.pregnancyexercise.co.nz/products/fit2birthmum/. Imechukuliwa mara ya mwisho 3.06.2020
Malposition and malpresentantio. https://www.gfmer.ch/Obstetrics_simplified/malpresentations_and_malposition.htm. Imechukuliwa 04.06.2020
Ocipitalposterior.https://www.uptodate.com/contents/occiput-posterior-position. Imechukuliwa 04.06.2020
Pushing the baby out.https://www.whattoexpect.com/pregnancy/labor-and-delivery/childbirth-stages/pushing-and-delivery.aspx. Imechukuliwa 06.06.2020
NCBI. When and where to puch. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC1804305/. Imechukuliwa 06.06.2020
Pushing during labor more isint better. https://www.parents.com/pregnancy/giving-birth/labor-and-delivery/pushing-during-labor-more-isnt-better/. Imechukuliwa 06.06.2020