Mwandishi:
ULY CLINIC
6 Juni 2020 14:51:59
Namna sahihi ya kusukuma mtoto
Kuvuta pumzi kwa kina ni jambo la kwanza linachotakiwa ili kusaidia juhudi za kusukuma mtoto. Kwenye hatua ya pili ya leba (uchungu) utatakiwa kusukuma mtoto ili aweze kutoka kirahisi, kumbuka ili kupata nguvu zenye ufanisi, unatakiwa kuvuta pumzi kwa kina kiasi na si kwa kina sana.
Ni nini kinatokea endapo utavuta hewa kwa kina?
Kuvuta hewa kwa kina husaidia kushusha chini ukuta wa chini ya kifua unaoitwa dayaframu. Ukuta huu unaposukumwa chini kwa kuvuta hewa kwa kina, husaidia kusukuma kizazi na mwishowe kusukuma mtoto ili atoke nje. Angalia picha namba moja kuona ukuta wa dayaframu na jinsi unavyobadilika wakati ukivuta hewa(picha namba 1a na b)
Ukuta wa dayaframu ukishuka chini zaidi kama kwenye picha 1b, huzifanya mbavu kubana hivyo kupelekea misuli ya tumbo kufanya kazi vema kusukuma mtoto. Ukivuta hewa kwa kina kisha kushika pumzi, unatanua eneo la ndani ya kifua, hivyo unafanya misuli ya tumbo iweze kufanya kazi kwa ufanisi kusukuma mtoto. Kuvuta pumzi kisahihi ni kitu cha kwanza kinachotakiwa kuleta ufanisi kwenye zoezi la kujifungua wakati huu wa hatua ya pili ya leba. Ukizingatia hili, utazuia kutumia muda mrefu wa kujifungua na kupata maumivu ya muda mfupi.
Sakafu ya nyonga huwa na matundu matatu, tundu la haja kubwa, tundu la uke na tundu la mkojo kama inavyoonekana kwenye picha namba 2. Unapokuwa unafanya jitihada za kusukuma mtoto, unaweza kujikuta umetoa haja kubwa au ndogo au kujifungua kutokana na kugandamizwa kwa maeneo ya ndani ya matundu haya.
Unapopofanya jitihada za kusukuma mtoto
Unapopofanya jitihada za kusukuma mtoto hakikisha unafanya mambo yafuatayo ili kupata ufanisi zaidi;
Vuta pumzi kwa kutumia pua na toa pumzi kwa kutumia mdomo
Vuta pumzi mara nyingine na kisha ishike, bila kuiachia sukuma hewa hiyo ndani ya kifua kwenda juu kwa taratibu kisha kuelekea chini ya mgongoni. Nguvu inayozalishwa napofanya hivi husukuma mtoto kutoka nje.
Kwanini mama hupata hamu ya haja kubwa anapokuwa kwenye uchungu?
Wakati mama anasukuma mtoto, njia ya haja kubwa hufunguka kwa sababu misuli ya sakafu ya nyonga husinyaa taratibu katika sehemu ya nyuma hivyo hugandamiza kifuko cha kutunza kinyesi na hii huruhusu kinyesi kutoka nje.
Wakati huu mwanamke anapotaka kusukuma kwa ajili ya kujifungua, kutoka kwa kinyesi hufanya kizuizi cha mtoto kupita kwenye tundu la uke. Hata hivyo mama atajifungua kutokana na jitihada kubwa za misuli ya tumbo na dayaframu kusukuma na kushinda kizuizi hiko.
Ili kuzuia kutumia nguvu nyingi pasipo sababu na kuufanya mwili wako uchoke, kuishiwa nguvu na kulegea na hatimaye kutumia muda mrefu wa kujifungua fanya mambo yafuatayo unapokuwa hatua hii ya kujifungua;
Pumzisha mwili wako kwa kuweka mgongo chini ya kitanda
Mabega na kichwa kilale kwenye mto
Usibane magoti au kuyakaza kwa namna yoyote ile
Pumzisha mikono kwenye godoro ulilolalia, usishike chochote hata kama ni kingo za kitanda chako
Namna ya kuzuia kusukuma mtoto kabla ya wakati wa kusukuma kufika
Wakati mwingine, unaweza kuhisi haja ya kusukuma mtoto. Kama hali hiyo ikitokea kabla ya wakati wake kama vile inavyotokea kwenye hatua ya kwanza ya leba mwishoni, hali hiyo inaweza kuzuiwa kwa kufanya mambo yafuatayo;
Kuvuta pumzi kwa kina kiasi kupitia pua ikifuatiwa na kuvuta hewa pasipo kina na ikifuatiwa na kuitoa pumzi kwa muda mrefu. Rudia hivi mpaka haja ya kusukuma iishe.
Njia hii husaidia kuzuia ukuta wa dayaframu usiongeze shinikizo ndani ya tumbo la uzazi.
Nini hatari ya kusukuma mtoto kabla ya wakati kufika?
Kuchanika kwa kizazi
Kuchanika kwa uke
Kutokwa na damu nyingi
Kuvimba kwa njia ya uzazi
Majeraha kwa mtoto haswa kwenye ubongo
Daktari au nesi atakuambia wakati gani wa kusukuma ili kuzuia mambo haya kutokea.
Muulize daktari wako siku zote endapo mazoezi haya yatakufaa kulingana na hali ya afya yako.
ULY clinic inakukaribisha kwa ushauri na Tiba. Wasiliana nasi kupitia namba za simu au bonyeza kitufe cha ‘Pata Tiba’ chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
1 Oktoba 2021
Rejea za mada hii;
American Pregnancy Association. Sleeping positions during pregnancy. Imechukuliwa 28.04.2020
National Sleep Foundation. The best position for sleep during pregnancy.Imechukuliwa 28.04.2020
National Posture Institute. Incorporating NPI’s 4 points of posture during pregnancy and postpartum. Imechukuliwa 28.04.2020
https://www.pregnancyexercise.co.nz/products/fit2birthmum/. Imechukuliwa mara ya mwisho 3.06.2020
Malposition and malpresentantio. https://www.gfmer.ch/Obstetrics_simplified/malpresentations_and_malposition.htm. Imechukuliwa 04.06.2020
Ocipitalposterior.https://www.uptodate.com/contents/occiput-posterior-position. Imechukuliwa 04.06.2020
Pushing the baby out.https://www.whattoexpect.com/pregnancy/labor-and-delivery/childbirth-stages/pushing-and-delivery.aspx. Imechukuliwa 06.06.2020
NCBI. When and where to puch. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC1804305/. Imechukuliwa 06.06.2020
Pushing during labor more isint better. https://www.parents.com/pregnancy/giving-birth/labor-and-delivery/pushing-during-labor-more-isnt-better/. Imechukuliwa 06.06.2020