Nephrotic syndrome-Figo kupoteza protini kwa wingi
​
Imeandikwa na madaktari wa uly clinic
​
Utangulizi
​
Nephrotic syndrome ni tatizo la figo linalo sababisha figo kupoteza protini kwa wingi kupitia mkojo
Tatizo hili mara nyingi husababishwa na uharibifu unaotokea kwenye mkusanyiko wa mishipa midogo katika figo(glomerula) inayofanya kazi ya kuchuja damu na kuondoa uchafu katika damu inayopita maeneo hayo.
Tatizo la nephrotic syndrome hutoa dalili za mwili kuvimba haswa kwenye maeneo ya kanyagio, kifundo cha mguu na miguu mzima. Kuvimba huku huongeza hatari ya kupata matatizo mengine ya kiafya.
Matibabu ya nephrotic syndrome huelekezwa kutibu kisababishi kwa kutumia dawa.
Ni muhimu kujua kwamba tatizo hili huweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya mara kwa mara na damu kuganda mwilini. Unaweza kushauriwa kuhusu chakula na madawa ili kuzuia madhara hayo na mengine yanayotokana na tatizo hili.
Dalili
Dalili na viashiria vya tatizo la nephrotic syndrome huwa ni pamoja na;
-
Kuvimba sana maeneo yanayozunguka jicho, kifundo cha mguu na miguu
-
Mkojo kuwa na povu- hutokana na kiwango kikubwa cha protini kweney mkojo.
-
Kuongezeka uzito- kutokana na mwili kujaa maji
Mwone daktari endapo unapata dalili ambazo zinakupa hofu, ni vema ukaonana na daktari wako , unaweza kuuliza maswali kupitia mawasiliano yetu chini ya maelezo haya
Visababishi vya nephrotic syndrome
Kwa kawaida tatizo hili husababishwa na uharibifu katika mishipa midogo ya damu iliyokusanyika kwa pamoja na kutengeneza chujio lijulikanalo kama glomerula.
Glomerula huchuja damu inayopita kwenye figo, kwa kufanya hivi huondoa sumu na majimaji yaliyozidi mwilini. Glomerula yenye afya njema huwa haichuji protini kwenye kwenye mkojo, hutunza protini katika damu ambayo inahitajika kutunza kiwango sahihi cha maji mwilini. Endapo kuna uharibifu katika glomerula basi huruhusu kiwango kikubwa cha protini kupotea katika mkojo. Na kusababisha tatizo la nephrotic syndrome.
​
Matatizo mengine yanayoweza kuharibu glomerula na kusababisha kiwango kikubwa cha protini kupotezwa na figo-nephrotic syndrome ni;
Tatizo la Mabadiliko kidogo kwenye chembe figo-minimal change disease
​
Huongoza kwa kusababisha tatizo la kupoteza kiwango kikubwa cha protini kupitia figo kwa watoto, tatizo hili hupelekea figo kufanya kazi kusiko kawaida, chembe za figo zinapochukuliwa na kuchunguzwa huonekana zinamabadiliko kidogo ama zina fanana na chembe asilia. Hakuna maelezo ya kutosha kwa nini figo inashindwa kufanya kazi ipasavyo kwa sababu hii.
Makovu kwenye glomerula
​
Kwa lugha nyingine ni focal segmental glomerulosclerosis, huwa na sifa za makovu yaliyosambaa sehemu kadha wa kadha kwenye chujio la mkojo-glomerula. Tatizo hili linaweza kusababishwa na magonjwa ama matatizo ya Kurithi-kijeni au linaweza kutokea pasipo sababu inayojulikana.
Kunenepa kuta za glomerula.
​
Kwa jina jingine Membranous nephropathy, kuta za chujio la figo - glomerula huwa nene kuliko kawaida. Sababu za kuongezeka kwa unene wa kuta hazijulikani. Lakini wakati mwingine huambatana na magonjwa kama homa ya ini inayosababishwa na kirusi hepatitis B, malaria-Homa ya mbu, lupus na aina fulani za saratani.
Ugonjwa wa figo kutokana na kisukari
Ugonjwa wa kisukari unaweza kupelekea kuhalibiwa kwa figo pamoja na glomerula
​
lupus inayosambaa mwilini
Ugonjwa sugu wa michomo kwenye mwili unaoweza kusababisha mabadiliko katika figo
Tatizo la amyloidosis-
Ni tatizo linalotokea endapo kiwango cha protini kinachoitwa amyloid kimerundikwa katika ogani mbalimba za mwili ikiwemo figo. protini hizi endapo zitajirundika kwenye chujio la figo huweza kusababisha uharibifu kwenye chujio hili.
Baadhi ya aina za kufeli kwa moyo kama kunako sababishwa na moyo ku kandamizwa upande wa kulia wa moyo huweza kusababisha tatizo la figo kutoa kuwango kikubwa cha protini kuliko kawaida.
Kuganda kwa damu kwenye mishipa ya veini ya figo
Kuganda kwa damu kwenye mishipa ya vein huweza kusababisha kiwango cha protini kupotea kwa wingi.
​
Vihatarishi
Mambo yanayoweza kusababisha tatizo la nephrotic syndrome ni kama;
​
Magonjwa Fulani yanayoongeza hatari ya kuharibu figo
-
Magonjwa kama kisukari, lupus na amyloidosis, ugonjwa wa mabadiliko kiasi kwenye figo na magonjwa mengine ya figo
Matumizi ya Madawa fulani
-
Madawa aina ya NSAIDS kama aspirini na madawa yanayotumik kupambana na maambukizi.
​
Maambukizi aina Fulani
-
Maambukizi ya VVU-UKIMWI, homa ya manjano inayosababishwa na kirusi cha hepatitis B, C na malaria.
-
Imeandikwa na madaktari wa ULY-Clinic
​
Madahara
​
-
Kuganda kwa damu- figo kutochuja protinikwa umakini huweza kusababisha kupotea kwa protini zinazotumika kuzuia kuganda kwa damu.
-
Kiwango kikubwa cha lehamu kwenye damu- kiwango cha protini kinapopungua katika damu kutokana na kupotea kwenye mkojo husababisha ini kuanza kutengeneza protini ili kukabili upungufu huo, katika harakati za utengenezaji wa protini lehamu huzalishwa na kuongezeka katika damu. Lehamu mbaya huongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
-
Utapiamlo- kupotea kwa kiwango kikubwa cha protini katika mwili hupelekea mtu kuwa na utapiamlo. Uzito kupungua hutokea ila kunaweza kufichwa kwa kuwa mwili huvimba kwa kujaa maji. Watu hawa pia huwa na upugnufu wa damu(anemia) na kiasi kidogo cha vitamin D na madini ya kalisium.
-
Shinikizo la juu la damu-kuharibika kwa glomerula husababisha kuongezeka kwa uchafu wa uremia kwenye damu, sumu ama uchafu huu huwea kusababisha kupanda kwa shinikizo la damu.
-
Figo kufeli ghafla kufanya kazi- kama figo ikifeli kuchuja damu na kuondoa uchafu, sumu hukusanyika katika damu kwa haraka. Unaweza kuhitaji mashine za kusaidia figo kuchuja sumu na kuondoa maji ya ziada
-
Magonjwa sugu ya figo-tatizo la kupoteza protini kwa wingi kwenye figo huweza kusababisha kuendelea kuharibika kwa figo jinsi mda unavyosonga, kama kazi za figo zinapungua chini ya kiwango kinachotakiwa utahitaji mashini za kuweza kukusaidia kufanya kazi za figo. Wakati mwingie utahitaji kuwekewa figo nyingine kutoka kwa mtu mwingine.
-
Maambukizi- watu wenye tatizo hili huwa na kihatarishi cha kupata maambukizi kwa sababu hupoteza protini ambazo hutumika kutengeneza kinga za mwili.
-
Vipimo na utambuzi
-
Kipimo cha mkojo
-
Kinaweza kutambua madhaifu kwenye mkojo kama kiwango kikubwa cha protini kama unatatizo la kupoteza protini kwa wingi, unaweza kuombwa kukusanya mkojo ndani ya masaa 24 ili kuangalia idadi ya protini iliyopotea kwa muda wa masaa 24.
​
Vipimo
Kipimo cha damu
​
-
Kama una tatizo la kupoteza protini kwa wingi kwenye mkojo basi kiwango cha protini aina ya albumin kwenye damu huwa chini na kiwango cha protini zingine kwenye damu kwa ujumla huwa chini. Kiwango cha lehamu huongezeka. Kiwango cha creatinine na urea kinaweza kupimwa ili kutambua kwa namna gani figo imeathiliwa na tatizo hili.
-
Kukatwa kinyama kwenye figo kwa ajili ya kipimo cha biopsy
-
Kinyama hukatwa na kupimwa ili kujua mabadiliko katika glomerula na chembe nyingine kwenye figo. Sindano maalumu huingizwa kupitia kwenye ngozi hadi kwenye figo na kuchukua kinyama hicho tayari kwa kipimo cha biopsy.
Matibabu
-
Matibabu ya tatizo la kupoteza protini kwa wingi katika mkojo huhusisha kutibu chanzo cha ugonjwa huo. Daktari wako anaweza kukupa dawa kadha wa kadha kwa ajili ya kuzuia dalili na viashiria ama madhara yaliyotokana na tatizo hili.
​
Madawa haya huwa kama;
-
Madawa ya kushusha shinikizo la damu-dawa aina ya ACE hupungusha shinikizo la damu la juu na pia hpunguza kiasi cha protini kinachotolewa na figo. Captopril, enalapril na benazepril huwa kwenye kundi hili. Pia kuna kundi jingine la ARB ambaro hufanya kazi inayofanana na kundi hili, dawa hizo ni losartan na valsartan.
-
Dawa za kupunguza maji- vidonge vya kupunguza maji mwilini husaidia kupunguza maji kwa kuongeza uwezo wa figo kuchuja maji kwenye damu. Kwenye kundi hili dawa kama furosemide na aldactone hutumika.
-
Dawa za kupunguza kiwango cha lehamu mwilini-madawa ayanayoitwa statins huweza kukusaidia kupunguza kiwango cha lehamu kwenye damu na hivo kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyona mishipa ya damu na kupunguza kufa kutokana na na kushikwa kwa moyo. Kundi hili lina dawa kama atovarstatin, simvastatin, lovastatin, fluvastatin na pravastatin.
-
Dawa za kuyeyusha damu- madawa yanayoitwa antcoagulant hutumika kuyeyusha damu na kupunguza hatari ya damu kuganda, damu kuganda huweza kusababisha matatizo makubwa mwilini. Madawa yaliyo kwenye kundi hili ni kama vile heparine na warfarin.
-
Madawa ya kupunguza kinga ya mwili- madawa ya kushusha kinga ya mwili kama corticosteroid huweza kushusha kinga ya mwili na huweza kupunguza michomo ambayo huambatana na magonjwa ya figo kama ugonjwa wa Mabadiliko kiasi kwenye chembe figo-minimal change disease.
​
​
Toleo la 3
Imeboreshwa 7/1/2019