top of page
Writer's pictureDr.Sospeter Mangwella, MD

Chakula cha mgonjwa wa seli mundu| ULY CLINIC

Seli mundu ni ugonjwa unaotokana na udhaifu katika umbo la chembe nyekundu ya damu, ugonjwa huu hurithiwa kutoka kwa baba na mama wenye vinasaba vya ugonjwa huu. Seli mundu ikifahamika pia kwa jina la ugonjwa wa sickle seli huathiri sana watu wenye asili ya Afrika na Amerika ya kusini.


Dalili za mbalimbali huonyeshwa na wagonjwa hawa na kubwa ikiwa ni maumivu ya mara kwa mara pale kutokuwa vema na maambukizi ya mara kwa mara.

Kutokana na dalili hizo, mgonjwa wa seli mundu huwa na mahitaji maalumu mengi hata hivyo katika makala hii utajifunza kuhusu mahitaji maalumu ya lishe.

Kwa kufahamu mahitaji haya itakupa mbinu mbalimbali za kuishi au kuwasaidia wagonjwa wenye tatizo hili la wasipatwe na madhara kutokana na kukosa virutubisho sahihi mwilini mwao.

Chakula kina uwezo mkubwa wa kubadili afya ya mwathirika wa seli mundu na kumfanya aishi maisha yenye afya njema zaidi. Tumia au mwache mgonjwa atumie chakula anachohitaji, kumbuka mgonjwa wa seli mundu huwa na vipindi vya kukosa hamu ya kula, hivyo kumpa uhuru wa kuchagua vyakula mbalimbali kati ya virivyoorodheshwa kwenye makundi hapa chini kutamfanya aendelee kula zaidi vyakula anavyopenda.


Makundi maalumu ya chakula kwa mgonjwa wa seli mundu anayopaswa kutumia na mfano wake

Vyakula vya nafaka visivyokobolewa mfano, mkate, mtama, mahindi, Mchele, uwele n.k

Umuhimu wake

  • Huwa na nyuzinyuzi ambazo huzuia haja ngumu na kupunguza kiwango cha rehamu kwenye damu

  • Huwa na madini ya foleti husaidia mwili kutengeneza chembe nyekundu za damu,

  • Huwa na vitamin B husaidia mwili kutengeneza nguvu

  • Huwa na madini ya magneziamu ambayo huimarisha mifupa

  • Huwa na madini ya seleniumu ambayo huimarisha mfumo wa kinga mwilini, tafiti zinaonyesha pia huzuia kuvunjwa kwa chembe nyekundu za damu

Mboga za majani ya rangi ya kijani kuelekea nyeusi au machungwa, mfano spinachi, karoti, brokoli, nyanya, maharagwe ya kijani na saladi ya mboga mboga

Umuhimu wake

  • Huwa na nyuzinyuzi ambazo hufanya ngozi iwe na afya njema

  • Huwa na madini ya foleti

  • Huwa na vitamin A ambayo hufanya ngozi na macho yawe na afya njema na kukukinga na magonjwa

  • Huwa na Vitamin C ambayo husaidia kuponya vidonda na kufanya fizi ziwe na afya njema

  • Huwa na Madini ya potasiamu yanayofanya mwili uwe na shinikizo la damu la kawaida

Matunda kama machungwa, ndizi, tufa, zabibu, matunda madogomadogo, kiwi.


Matunda haya ni vema yakaliwa na nyuzinyuzi zake na hata kama yakitengenezewa juisi ni vema isichujwe ili kupata virutubisho vyote vya nyuzinyuzi, vitamin mbalimbali na madini kama yalivyoorodheshwa hapo juu.

Maziwa, maziwa mtindina siagi huwa na madini ya kalisiamu na vitamin D, pia huwa na madini ya potasiamu yenye umuhimu katika mwili kama ilivyoelezewa hapo juu.


Nyama na maharagwe mfano Kuku, kitimoto, ng’ombe, karanga, mbaazi na maharagwe


Umuhimu

  • Huwa na Protini kwa wingi na madini ya zinki yanayosaidia ukuaji na kuupa mwili nguvu

  • Huwa na madini chuma yanayosaidia chembe nyekundu ya damu kubeba oksijeni

  • Huwa na mafuta ya omega 3 haswa samaki na baadhi ya mbegu za karanga ambayo hupunguza kiwango cha rehamu mbaya kwenye damu na kukuondoa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.


Mafuta, tumia mafuta kutoka kwenye mimea sana haswa mafuta ya mbegu za mzeituni, kitani, ufuta, alizeti, karanga. Mafuta haya huwa na Vitamin E ambayo hutoa sumu kwenye seli na kufanya isihi muda mrefu, huwa na omega 3 hasa mafuta ya mbegu za kitani, mbegu za kanola na maboga

Mambo mengine ya kukumbuka


  • Kunywa vimiminika vya kutosha kama juisi na maji ili kuzuia kuishiwa maji mwilini na haja ngumu

  • Usitumie vinywaji vyenye kafeini

  • Beba chakula unapokwenda maeneo ambayo huwezi kupata chakula kirahisii

  • Kula vyakula kutoka kwenye makundi 3 hadi manne ya chakula

  • Tumia maziwa yanayoongeza madini ya kalisiamu mwilini

  • Wasiliana na daktari wako endapo kuna uhaja wa kutumia vidonge vya vitamin D kukabiliana na upungufu.

  • Madini ya seleniamu husaidia kupunguza vipindi vya maumivu ya seli mundu, madini haya yanayopatikana kwa kiwango kikubwa kwenye nyama ya kitimoto, ng’ombe, bata mzinga, kuku, samaki na mayai, hupatikana pia kwenye vyakula vya mbegu kama maharagwe na karanga kwa kiwango kidogo.

Rejea za makala hii


  1. Boston Medical Center. Eating to be Well with Sickle Cell Disease. https://www.bmc.org/sites/default/files/About_Us/Features/Sickle_Cell_Disease_Treatment_at_BMC/field_Attachments/SickleCellDisease-EatingHealthy.pdf. Imechukuliwa 15.11.2020

  2. Emília Delesderrier etal .Selenium Status and Hemolysis in Sickle Cell Disease Patients. https://www.mdpi.com/2072-6643/11/9/2211/htm. Imechukuliwa 15.11.2020

  3. Sickle cell anemia news. https://sicklecellanemianews.com/2019/10/17/sickle-cell-disease-diet-selenium-research/. Imechukuliwa 15.11.2020

  4. Kids eating right. Nutrition for the Child with Sickle Cell Anemia. https://www.eatright.org/health/allergies-and-intolerances/food-intolerances-and-sensitivities/nutrition-for-the-child-with-sickle-cell-anemia#. Imechukuliwa 15.11.2020

  5. NHS. Food high in vitamin D. https://www.nhs.uk/conditions/vitamins-and-minerals/vitamin-d/. Imechukuliwa 15.11.2020

  6. Sickle cell society. Nutrition in sickle cell disease. https://www.sicklecellsociety.org/nutrition-in-sickle-cell-disease/. Imechukuliwa 15.11.2020

  7. NIH. Selenium. https://ods.od.nih.gov/factsheets/Selenium-HealthProfessional/#. Imechukuliwa 15.11.2020

1,975 views0 comments

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page