Hili ni swali ambalo wanawake wengiwajawazito wamekuwa wakijiuliza na wakihofia kuhusu maambukizi ya UTI kwenye ujauzito. Swali hili limejibiwa vizuri hapa chini.
Je UTI inaweza kutoa mimba?
Jibu rahisi ni kwamba UTI inaweza kusababisha mimba kutoka lakini si kirahisi sana. Si rahisi kwa sababu maambukizi ya UTI huwa kwenye mfumo wa chini wa mkojo hivyo hauna mahusiano moja kwa moja na mfuko wa uzazi.
Hata hivyo kuwa na UTI kwenye ujauzito huongeza hatari ya mimba kutoka pamoja na kujifungua kabla ya wakati kutokana na kupasuka mapema kwa chupa ya uzazi, sababu inaweza kuwa kati ya madhara ya UTI(sepsis) au matumizi ya baadhi ya dawa kutibu UTI kipindi hiki.
Ni wakati gani maambukizi ya UTI yanaweza kusababisha mimba kutoka?
Maambukizi ya UTI yanaweza kusababisha mimba kutoka endapo bakteria wanaosababisha UTI wamepanda na kuingia kwenye mfumo wa juu wa mkojo yaani kutoka kwenye kibogu cha mkojo kwenda kwenye figo kupitia mirija ya ureter. Vimelea hawa wakifika kwenye figo hupata upenyo wa kuingia kwenye mishipa mikuu ya damu na hivyo kusambaa kwenye damu na kuamsha tatizo linaloitwa sepsis. Sepsis hutokea pale mwili unapoiamsha kinga za mwili kupambana na maradhi kwenye damu, hali hii hutishia maisha kwa sababu mtu huwa mgonjwa sana na mwili pia huchoka na wakati huu mimba inaweza kutoka bila ugumu wowote.
Vihatarishi vya kupata Sepsis kutokana na UTI
Baadhi ya vihatarishi vya kupata sepsis ni;
Kuwa na umri mkubwa Zaidi(uzee) au kuwa na umri chini ya mwaka mmoja
Kuwa mjamzito
Kuwa na magonjwa sugu kama kisukari, UKIMWI na magonjwa ya figo, mapafu na saratani
Kuwa na kinga za mwili zilizo chini Zaidi
Maambukizi gani mengine yanaweza kupelekea mimba kutoka?
Yapo maambukizi mengi yanayoweza kupelekea mimba kutoka, maambukizi mengi ni yale yanayogusa mfumo wa uzazi, hata hivyo maambukizi ya nje ya mfumo wa uzazi pia yanaweza kupelekea tatizo la mimba kutoka. Unaweza kupata maambukizi haya kabla au baada ya ujauzito na yakapalekea mimba kutoka. Baadhi ya maambukizi ni; (bofya kusoma zaidi)
Namna ya kujikinga na mimba kutoka kutokana na maambukizi ya UTI
Endapo una UTI kwenye ujauzito ni vema ukazingatia kanuni za kiafya kwa kupata matibabu yanayostahili kutoka kwa daktari wako. Kumbuka baadhi ya dawa za kutibu UTI zinaweza kusababisha mimba kutoka, hivyo tumia dawa sahihi kwa umri sahihi wa ujauzito. Ili kujikinga kupata UTI na mimba kutoka, ULY CLINIC inakushauri kufanya mambo yafuatayo;
Kunywa maji ya kutosha- hii itasaidia kusafisha bakteria kwenye mfumo wako wa mkojo
Kula mlo kamili- hii itasaidia kupata virutubisho muhimu kwenye mwili wako na hivyo kuimarisha kinga za mwili zinazopambana na maradhi
Kabla na mara baada ya kufanya ngono kojoa mara moja- Hii itasaidia kusafisha njia ya mkojo na kuondoa bakteria wanaosababisha UTI
Kila baada ya masaa mawili hadi matatu, kojoa unapopata hamu ya kukojoa ili kusaidia kusafisha mfumo wa mkojo
Tumia kondomu endapo unafanya mapenzi na mtu mwenye UTI au ukiwa na wapenzi wengi
Jisafishe vema maeneo ya uke na njia ya haja kubwa ili kuzuia kujiambukiza, ukiwa unasafisha njia ya haja kubwa, safisha kutoka mbele kwenda nyuma huku mkono upo upande wa nyuma.Hii itakusaidia kuepuka kupeleka kinyesi na majimaji yanayotoka kwenye njia ya haja kubwa kwenda ukeni na njia ya mkojo.
Tumia dawa ya kutibu UTI kama utakavyoshauriwa na daktari wako, usitumie dawa bila ushauri wa daktari. Kumbuka wakati mwingine ni vema kutotumia dawa kabisa endapo maambukizi yanaisha kwa njia zilizotajwa hapo juu.
Soma kala zingine zaidi zilizoorodheshwa hapa chini kuhusu ujauzito;
Rejea za mada hii
Flavia Ghouri. Urinary tract infections and antibiotic use in pregnancy - qualitative analysis of online forum content. https://bmcpregnancychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-019-2451-z. Imechukuliwa 3.1.2021
Anne C C Lee etal. Screening and treatment of maternal genitourinary tract infections in early pregnancy to prevent preterm birth in rural Sylhet, Bangladesh: a cluster randomized trial. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/26643558/. Imechukuliwa 3.1.2021
Lara A. Friel , MD, PhD. MDS manual. Infections During Pregnancy. https://www.msdmanuals.com/home/women-s-health-issues/pregnancy-complicated-by-disease/infections-during-pregnancy. Imechukuliwa 3.1.2021
Jameson JL, et al., eds. Sepsis and septic shock. In: Harrison's Principles of Internal Medicine. 20th ed.
Hall JB, et al. Sepsis, severe shock, and septic shock. In: Principles of Critical Care. 4th ed. New York, N.Y.: The McGraw-Hill Companies; 2015.
Bladder infection (urinary tract infection—UTI) in adults. (n.d.). https://www.niddk.nih.gov/health-information/urologic-diseases/bladder-infection-uti-in-adults#i. Imechukuliwa 3.1.2021
Glover, M., Moreira, C. G., Sperandio, V., & Zimmern, P. (2014, March). Recurrent urinary tract infections in healthy and nonpregnant women. Urological Science, 25 (1), 1–8. https://www.sciencedirect.com/science/article/pii/S1879522614000037. Imechukuliwa 3.1.2021
Commentaires