top of page
Writer's pictureDr.Sospeter Mangwella, MD

Kuwashwa ngozi baada ya kuoga| ULY CLINIC

Updated: Dec 10, 2021



Kuwashwa ngozi baada ya kuoga ni hali inayotokea kwa baadhi ya watu, hali hii inaweza kusababisha mtu kuogopa kugusa maji. Makala hii imeelezea baadhi ya visababishi na magojnwa yanayofahamika kusababisha mwili kuwasha baada ya kuoga.


Ni nini husababisha ngozi kuwasha


Baadhi ya sababu zinazosababisha ngozi kuwasha ni;



Kukauka kwa ngozi


Unapokuwa unaoga, maji na sabuni huondoa mafuta asili ya ngozi na kusababisha ikauke na kuwasha. Ngozi iliyokauka huwa na tabia ya kuvuta na muwasha hususani mara tu baada ya kuoga. Matumizi ya sabubi au vitakasa vinavyoodoa sehemu ya juu ya ngozi na mafuta husababisha ngozi ikauke.


Eczema


Huu ni ugonjwa wa mzio wa ngozi, husabisha ngozi kukauka, kuwasha, kuwa nyekundu pamoja na harara au vipele kwenye ngozi.


Dalili za eczema zinaweza kuwa nyingi na kali zaidi hasa mara baada ya kuoga, hii ni kwa sababu wakati huu ngozi huwa imeondolewa mafuta yake ya asili. Sabuni kali zenye kemikali na maji ya moto huweza kuamsha hali hii ya kuwashwa kwa ngozi.


Mwitikio wa ngozi kwenye vichokoza ngozi


Vichokoza ngozi ni vitu ambavyo vinasababisha mzio kwenye ngozi na hivyo kufanya iwashe. Baadhi ya vikereketa ngozi ni vitu unavyotumia wakati wa kuoga mfano;

  • Sabuni zenye marashi

  • Sabuni zinazokausha ngozi

  • Shampoo za kuoshea nywele zenye marashi au za kukausha ngozi

  • Na zingine ambazo zinakuletea miwasho


Mwitikio wa ngozi kwenye nguo unazotumia


Mavazi yaliyofuliwa kwa kutumia vitakasa vikali vyenye kuleta mzio wa ngozi huweza kusababisha kuwasha kwa ngozi kwa watu ambao wana mzio wa kemikali hizo zilizotumika.


Kama unapata mzio wa ngozi ya aina hii ni vema kuepuka kufua nguo kwa kemikali hizo. Tumia vitakasa nguo vingine ambavyo ni salama kwa ngozi yako.


Magonjwa mengine ya mwili ambayo ni;

  • Polycythemia Vera- ni ugonjwa wa uboho wa mifupa unaopelekea uzalishaji wa chembe nyekundu za damu nyingi kupita kiasi(husababisha kuwa na damu nyingi). Mbali na kuwashwa mwili wakati wa kuoga hupelekea dalili zingine mbalimbali ambazo ni; maumivu ya kichwa, kubadilika kwa uono, maumvu ya kifua, kutokwa na damu kirahisi, kuvimba kwa ini na bandama

  • Hodgkin Lymphoma- hii ni saratani ya mitoki, watu wenye saratani hii huvimba maeneo yenye mitoki kama shingoni, maeneo ya kinena, kwapa na ndani ya kifua. Mbali na ngozi kuwasha dalili zingine ni; maumivu ya kichwa, kubadilika kwa uono wa macho, maumvu ya kifua, kutokwa na damu kirahisi, kuvimba kwa ini na bandama

  • Cholinergic Urticaria- ni aina ya magojnwa ya magonjwa ya kuvimba ngozi mara inapokutana na maji, huamshwa kwa maji ya moto au baridi, msongo wa mawazo, kujifunika mashuka mengi wakati wa usiku, joto, kupigwa mwanga wa jua, kula vyakula vyenye viungo vingi n.k

  • Aquagenic Urticaria- huleta dalili ya ngozi kuwasha pamoja na kutengeneza harara(ngozi kuvimba) kwenye ngozi mara ngozi inapoguswa na maji.

  • Idiopathic Aquagenic Pruritus- hutokea kwa nadra sana na husababisha miwasho ya ngozi bila kuleta harara kwenye ngozi mara baada ya maji kugusa ngozi


Matibabu


Matibabu mara nyingi yanahusisha kutumia sabuni na kupaka mafuta mazito yasiyo chokoza ngozi ili kurejesha unyevu kwenye ngozi. Mara nyingine inaweza isiwe rahisi kwako na ukahitaji kutumia dawa za kuzuia miwasho.


Mambo mengine muhimu unayowa fanya ili kukabiliana na tatizo hili ni;

  • Oga kwa muda mfupi sana. Tumia maji ya baridi au ya moto kiasi na oga kwa muda mfupi, usitumie nguvu kusugua ngozi yako ili kuzuia kuondoa ukuta wote na mafuta ya juu ya ngozi.

  • Epuka kuoga zaidi ya mara mbili kwa siku. Ukioga zaidi ya mara mbili kwa siku inamaanisha unatoa ukuta na mafuta ya asili yaliyo juu ya ngozi zaidi ya mara mbili na kupelekea ngozi kuwasha zaidi. Endpo unaoga zaidi ya mara mbili hakikisha kwamba hutumii sabuni au maji ya moto kwa sababu huwa na tabia ya kukausha ngozi pia fuata ushauri uliotolewa hapo juu.

  • Zuia kukogelea kwenye sinki la maji ya moto kwa muda mrefu wakati unaoga, mbali na kuzuia kukaa muda mrefu kwenye sinki, tumia sabuni zenye mafuta au mafuta ya kuogea kwenye maji ili kufanya ngozi yako iwe na unyevu.

  • Usikune ngozi yako inapowasha, hii itakusaidia usijeruhi ngozi na kufanya iwashe zaidi

  • Usitumie taulo, usifanye scrabu au kukausha ngozi kwa nguvu zaidi ili kuzuia kuchokoza ngozi hna miwasho

  • Usitumie vitakasa mwili vyenye spirit au pombe kwa sababu huchokoza ngozi na kufanaya iwashe

  • Unapokausha ngozi usikaushe kwa kufuta/kusugua bali kwa kubandika taulo kwenye ngozi na kutoa bila kutumia nguvu nyingi.

  • Tumia mafuta mazito au losheni ya krimu yasiyo na marashi kupaka ngozi mara baada tu ya kufuta ngozi yako.

  • Tumia viongeza unyevu kwenye hewa ili kuongeza unyevunyevu na kusababisha ngozi isiwashe

  • Usitumie sabuni au vitakasa nguo vikali kufua nguo zako haswa vile vinavyopelekea ngozi yako kuwasha


Wakati gani wa kumowna daktari


Mwone daktari endapo umefanya mambo yote hapo juu bila mafanikio kwa uchunguzi zaidi


Pia endapo una dalili hizi fika hospitali;

  • Endapo ngozi yako inabanduka, inatengeneza maghamba au kupata harara, unahitaji kufika hospitali kwa uchunguzi na matibabu zaidi

  • Una dalili za ugonjwa wa akili


Endelea kusoma kuhusu magonjwa mengine ya ngozi kwa kubonyeza hapa.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kiafya baada ya kusoma makala hii


Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa elimu na ushauri zaidi kwa kubonyeza Pata tiba au kupiga namba za simu chini ya tovuti hii


  1. Healthline. What causes itching after a shower? .https://www.medicalnewstoday.com/articles/326974. Imechukuliwa 20.11.2020

  2. Verywellhealth. 6 Reasons Why You Itch After Taking a Shower.https://www.verywellhealth.com/reasons-why-you-itch-after-taking-a-shower-83217. Imechukuliwa 20.11.2020

  3. Raedler LA. Diagnosis and Management of Polycythemia Vera: Proceedings from a Multidisciplinary Roundtable. Am Health Drug Benefits. 2014;7(7 Suppl 3):S36-47.https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/26568781/. Imechukuliwa 20.11.2020

  4. Ansell SM. Hodgkin Lymphoma: Diagnosis and Treatment. Mayo Clin Proc. 2015;90(11):1574-83. DOI:10.1016/j.mayocp.2015.07.005. https://linkinghub.elsevier.com/retrieve/pii/S0025619615005509. Imechukuliwa 20.11.2020

  5. Altrichter S, Wosny K, Maurer M. Successful treatment of cholinergic urticaria with methantheliniumbromide. J Dermatol. 2015;42(4):422-4. DOI:10.1111/1346-8138.12765. https://onlinelibrary.wiley.com/doi/abs/10.1111/1346-8138.12765. Imechukuliwa 20.11.2020

3,963 views0 comments

Recent Posts

See All

Comentarios


bottom of page