Watu wengi hudhani kuwa kila ugonjwa mwilini unahitaji dawa ili kuweza kujipona, hii si kweli kwani wanyama wengi duniani, miiili yao inauwezo wa ajabu wa kuweza kujiponya bila hata kutumia dawa. Fikiria wanyama wote wa porini, hawatumii dawa wala kupata chanjo lakini huugua na kupona wenyewe, je uwezo huo binadamu hanao?.
Makala hii imelenga kukuelimisha uwezo wa mwili wa binadamu kujiponya na nini cha kufanya ili mwili wako uwe na uwezo mkubwa zaidi pasipo kutumia dawa wala chanjo.
Mambo machache ya kufahamu
Ifahamike kuwa, kila baada ya siku 90 mwili wako hutengeneza chembe sahani mpya za damu na kila baada ya mwaka, chembe mpya zaidi ya bilioni hutengenezwa na kila baada ya miaka michache hutengeneza mifupa mipya. Mambo haya yote hutokea endapo utatendea haki mwili wako kwa kuupa unachostahili. Mwili umeutwa na chembe asilia ambazo zina uwezo wa kujizalisha na kutengeneza chembe hai mpya zenye uwezo wa kuleta uponyaji.
Ni vitu gani mwili unastahili kupata ili kuamsha uwezo wa mwili wako kujiponya wenyewe?
Ukifanya mambo sita (6) yaliyoorodheshwa hapa chini, utafanya mwili wako uwe na uwezo mkubwa zaidi wa kujiponya wenywe, ambayo ni;
Kuepuka msongo
Kunywa maji ya kutosha
Kulala masaa ya kutosha
Kula mlo kamili
Kufikiria kiafya
Kufanya mazoezi
Kuepuka msongo
Licha ya kuwa maisha yamejawa na mambo (vichocheo) yanayoleta msongo mwilini kwenye mwili wako, kama vile kufanya kazi kwa kukimbizana na muda au tarehe, kutafuta pesa, kuwazia mlo wa siku wa familia, kuwaza utapata wapi kodi ya nyumba au ada ya shule, kudaiwa na benki n.k, mambo haya yanabidi yasichukue nafasi kubwa katika maisha yako.
Pumzisha akili yako na usiwazie sana au kuyapa nafasi au muda mwingi. Kuwa na mpango na weka mikakati mizuri ya kufikia malengo yako, pia kuwa na malengo halisi ambayo yanaweza kufanyika ndani ya muda uliojipangia.
Epuka kuishi yaliyo nje ya uwezo wako, na wakati huo uwena mipango ya jinsi gani ya kujiongezea kipato cha halali bila kuudhuru mwili wako.
Kumbuka maisha si pesa tu, muda mwingi unapaswa kuwa na furaha hivyo epuka vitu vinavyokupa msongo mara kwa mara.
Msongo endelevu hupelekea homoni za msongo kuwa kwa muda mrefu kwenye damu, homoni hizi (cortisol, adrenalin na noradrenaline ) husabaisha kupungua kwa kinga za mwili, kuongezeka kwa shinikizo la damu, kisukari n.k. ni kweli huwezi kuzuia kuwa na msongo kabisa lakini usiwe na msongo wa muda mrefu.
Tumia njia mbaimbali za kuepuka msongo kwa kufanya mambo unayopenda, kufanya mazoezi au kuimba nyimbo n.k
Soma zaidi kuhusu msongo na namna ya kukabiliana nao ndani ya makala za ulyclinic kwa kubonyeza hapa
Kunywa maji ya kutosha
Maji husaidia kuweka sawia kemikali mbalimbali na kusafisha sumu kutoka kwenye damu, zinazotokana na chembe zinazokufa pamoja na chakula unachokula n.k. Ufanye mwili wako usikaukiwe maji kwa kuhakikisha unakunywa angalau glasi 8 za maji kila siku. Kunywa maji safi na salama, epuka maji yaliyotiwa kemikali ambazo zinahatari ya kudhuru chembe za mwili wako.
Soma zaidi kuhusu kiwango cha maji ya kunywa katika Makala zingine za ulyclinic kwa kubofya hapa au Hapa
Lala muda wa kutosha
Unapokuwa umelala, licha ya kuufanya mwili wako utulie, unaamsha mihimili mbalimbali homoni mwilini ili kuponya majeraha na kutengeneza chembe chembe mpya. Unapaswa kulala angalau masaa 8 kwa siku, hata hivyo inategemea umri wako.
Unapotaka kulala hakikisha umezima kila kitu ikiwa pamoja na simu, redio au TV, n.k na pia hakikisha kuna giza chumbani kwako unapolala. Giza huamsha mwili kuzalisha homon melatonin ambayo ni muhimu sana.
Kula mlo kamili
Kula chakula kutoka kwenye makundi matano (5) ya chakula yanayoshauriwa kiafya, chakula chako ni vema kikawa na vitu asilia (ambavyo havitajiwa kemikali) kwa kiasi kikubwa , mfano kuku wa kienyeji, mayai ya kienyeji, mboga za majani, matunda, vyakula vya nafaka visivyokobolewa n.k.
Fanya hivyo ili kuepusha kemikali mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwekwa kwenye vyakula vikiwa shambani au wakati wa kuhifadhi. Endapo unatumia vitu vilivyotiwa kemikali kama nyanya, matunda, mboga za majani n.k basi hakikisha umeviosha kwa maji ya kutosha kabla ya kupika au kula. Usipende kula vyakula vya kusindikwa kama soda, soseji n.k au vile vya kukaangwa kama chipsi n.k kwa kuwa huwa na sukari, chumvi na mafuta kwa wingi na ni hatari kwa afya yako.
Soma zaidi kuhusu mlo kamili kwenye Makala zingine zilizo ndani ya tovuti ya uly clinic kwa kubofya hapa na Kuhusu makundi ya vyakula bofya Hapa
Fikiria kiafya
Mwili wako kwa kawaida huitikia kwenye hisia na mawazo, ukiwa na hisia za hofu dhidi ya dalili uliyonayo au za kuugua, mwili wako utaugua hata kama hauna maambukizi.
Mfano kuna mtu alishiriki tendo la ndoa na mgonjwa wa UKIMWI bila kufahamu, baada ya muda marafiki zake waliona mtu huyu anajitenga na anakonda na kukohoa sana lakini hawakujua kwanini hawamuoni wakati wa kujisomea. Siku moja alitembelewa nyumbani na mmoja wa rafiki yake na kumuuliza kwanini haonekani, ndipo aliamua kuitoa siri kuwa allitembea na mwanamke mwathirika wa UKIMWI na sasa anahisi kuwa ana dalili za UKIMWI.
Rafiki huyu alimtia ujasiri na kumwambia hata kama umetembea na mwathirika, ni vema ukapima kujua hali yako na kisha kuanza maisha mapya, hata hivyo unawezekana umepata au la. Rafiki alimsindikiza kupima, majibu yalikuja kuwa NEGATIVE, alifurahi sana na baada ya mwezi hali ya mwili wake ilirejea kama awali na dalili zote zilipotea pasipo kutumia dawa.
Hii inatufundisha kuwa, mawazo HASI ya kujilaumu huharibu mwili mwili kwani hufanya mwili kuzalisha kemikali za msongoambazo hupelekea kinga ya mwili kushuka na pia kufanya uugue magonjwa mbalimbali, au kupata dalili ambazo hata ukipimwa ugonjwa hautaonekana.
Kuwa na mawazo chanya hata kama una ugonjwa ambao unasemekana kuwa hauponi kwani unapokuwa na mawazo chanya, mwili huzalisha chembe nyingi za ulinzi na kinga zenye uwezo wa kukuponya naam haya saratani, ugonjwa unaogopesha sana.
Madaktari kwa kutambua uwezo wa mwili kujiponya, hufanya tafiti kwa kutumia dawa zinazoitwa ‘placebo’ ambazo huwa ni kidonge kinachofanana na dawa lakini huwa hakina kiini cha dawa ndani yake( huweza kuwa na unga tu), cha kushangaza watu wenye magonjwa wanaopewa dawa placebo hupona kwa sababu tu huamini kuwa wamepewa dawa. Unapowaza mawazo CHANYA, unaamsha uzalishaji wa chembe za ulinzi na kinga ya mwili zaidi na kufanya uponyaji wa haraka kutokea.
Fanya mazoezi
Binadamu anapaswa kufanya kazi kila siku, kazi za kutoa jasho au kufanya mzunguko wa damu uwe mkubwa. Kutokana na mabadiliko ya maisha, watu wengi wanafanya kazi za ofisini zaidi(kazi za kukaa) kuliko zile za shamba au zinazohusisha kutumia nguvu nyingi. Hii imepelekea kukosa kufanya mazoezi na kutokea kwa magonjwa mengi yasiyo ya kuambukizwa. Hata hivyo kwa sasa watu wengi wanafanya mazoezi kwenye klabu mbalimbali za mazoezi.
Haijalishi ni wapi unafanya mazoezi au unafanya kazi gani, hakikisha unautumikisha mwili wako kwa kazi zinazotumia nguvu au kufanya mazoezi ya anaerobic na aerobic angalau mara tatu hadi nne kwa wiki ili kuamsha kinga za mwili pamoja na kuharakisha kutokea kwa uponyaji.
Rejea za makala hii
Programu ya mazoezi. https://www.ulyclinic.com/program-ya-mazoezi. Imechukuliwa 05.06.2021
Makundi ya vyakula. https://www.ulyclinic.com/makundi-ya-vyakula. Imechukuliwa 05.06.2021
Jiepushe na magonjwa kwa kula vema. https://www.ulyclinic.com/vidokezo-vya-kiafya/jiepushe-na-magonjwa-kwa-kula-vema. Imechukuliwa 05.06.2021
Kiasi cha maji ya kunywa kila siku kwa watoto. https://www.ulyclinic.com/vidokezo-vya-kiafya/kiasi-cha-maji-ya-kunywa-kila-siku-kwa-watoto. Imechukuliwa 05.06.2021
Maji. https://www.ulyclinic.com/maji. Imechukuliwa 05.06.2021
Muda unaotosha kulala. https://www.ulyclinic.com/vidokezo-vya-kiafya/muda-unaotosha-kulala. Imechukuliwa 05.06.2021
Msongo. https://www.ulyclinic.com/dalili-za-ugonjwa/Msongo . Imechukuliwa 05.06.2021
5 Easy Ways to Activate Your Natural Healing Ability. https://www.psychologytoday.com/intl/blog/mining-the-headlines/201401/5-easy-ways-activate-your-natural-healing-ability. Imechukuliwa 05.06.2021
Sleep Drive and Your Body Clock. https://www.sleepfoundation.org/circadian-rhythm/sleep-drive-and-your-body-clock. Imechukuliwa 05.06.2021
Harald Walach, et al. Placebo research: the evidence base for harnessing self-healing capacities. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/15630827/. Imechukuliwa 05.06.2021
Tobias Esch. [Self-healing in health-care: Using the example of mind-body medicine]. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/32274538/. Imechukuliwa 05.06.2021
Comments