Utokaji wa mate mengi wakati wa ujauzito hufahamika kama ptayalizm (ptyalism) au sialorea (sialorrhea). Wajawazito wenye tatizo hili hupata shida kumeza mate na huchagua kuwa na chombo cha kutemea mate au kitambaa cha kufutia mate hayo muda wote.
Baadhi ya wanawake wamekuwa wakitafuna bablishi au kumung'unya vipande vidogo vya barafu ili kudhibiti hali hii kwa muda hata hivyo uzalishaji wa mate unaweza kupungua wakati umelala
Mara nyingi tatizo hili huisha baada ya kupita kipindi cha kwanza cha ujauzito kupita yaani miezi mitatu ya mwanzo. Lakini baadhi ya wanawake wanaweza kuendelea na dalili hii mpaka wakati wa kujifungua.
Dalili zinazoambatana na utokaji mate kwenye ujauzito
Wajawazito wenye tatizo hili pia wamekuwa wakipata dalili zingine kama;
Hisia ya ladha mbaya kinywani
Kichefuchefu na kutapika kama wakimeza mate
Kuamka mara kwa mara baada ya kulala usiku
Kupaliwa mate wakati umelala
Nini kisababishi cha utokaji mate mengi wakati wa ujauzito?
Wanasayansi hawajaweza kutambua mpaka sasa ni nini kisababishi halisi cha utokaji mate mengi wakati wa ujauzito licha ya kuhusianisha tatizo hili na mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa ujauzito.
Kisayansi inafahamika kwa ujumla kwamba utoaji wa mate hudhibitiwa na mfumo wa neva. Uchochezi wa mfumo wa neva wa parasympathetic huamsha tezi za mate mdomoni na kusababisha uzalishaji mwingi wa mate. Hii ndio maana mpaka sasa baadhi maandiko ya kitiba yameshauri kutumia dawa za kutuliza mfumo wa fahamu wa kati jamii ya barbiturates na anticholinergics na baadhi ya dawa asili kama alpinia oxyphylla kudhibiti tatizo hili. Dawa hizi hazina matokeo ya kuridhisha na baadhi ya wataalamu wa afya na wanawake pia hawachagui kutumia njia hii kwa kuhofia madhara yanayoweza kutokea kwa watoto, haswa katika kipindi cha uumbaji wa viungo yaani kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.
Maelezo kuhusu matibabu ya dawa na yasiyo dawa, yanapatikana kwenye makala ya mate mengi katika ujauzito.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Unaweza kuwasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitina linki ya 'Pata tiba' au 'Wasiliana nasi' inayopatikana chini ya tovuti hii.
Rejea za mada hii;
Suzuki S, Igarashi M, Yamashita E, Satomi M. Ptyalism gravidarum. N Am J Med Sci. 2009;1(6):303-304.
Freeman JJ, Altieri RH, Baptiste HJ, Kao T, Crittenden S, Fogarty K, Moultrie M, Coney E, Kangis K. Evaluation and management of sialorrhea of pregnancy with concominant hyperemesis. J Natl Med Assoc. 1994;86:704–708.[PMC free article] [PubMed] [Google Scholar]
NCT. Excessive saliva in pregnancy. https://www.nct.org.uk/pregnancy/worries-and-discomforts/common-discomforts/excessive-saliva-pregnancy. Imechukuliwa 12/5/2022
Dental choice. Excessive Saliva During Pregnancy? Here’s What You Need to Know. https://www.dentalchoice.ca/excessive-saliva-during-pregnancy-heres-what-you-need-to-know/. Imechukuliwa 12/5/2022
VictoriaDe Braga, et al. Successful treatment of ptyalism gravidarum with clonidine hydrochloride: A case report. https://doi.org/10.1016/j.crwh.2022.e00409. Imechukuliwa 12/5/2022
Comments