Je vidonge vya majira huongeza uzito?
Naweza kutumia dawa za uzazi wa mpango kuongeza uzito?
Utangulizi
Upo usemi kwamba vidonge vya uzazi wa mpango(majira) huongeza uzito kwa wanawake wanaotumia vidonge hivi, makala hii imeandikwa mahususi kujibu maswali hapo juu na kukupa ufahamu zaidi kuhusu ongezeko la uzito kwa matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango kutokana na tafiti mbalimbali ziizofanyika.
Vidonge vya uzazi wa mpango ni nini?
Zipo njia mbalimbali za uzazi wa mpango, njia ya vidonge vya majira ni njia inayopenda zaidi na watu wengi kwa sababu ya faida yake kuu kwamba ni rahisi kuacha na kupata mtoto mara tu baada ya kuacha kutumia ukilinganisha na njia ya sindano ya depo.
Dawa za vidonge vya majira (OCP) ni dawa ambazo zimekuwa zikitumika hapa duniani kwa zaidi ya mika 40 sasa, dawa hizi huwa na mchanganyiko wa homoni ya progestin na estrogen na mpaka sasa kuna vizazi vitatu vya dawa za majira zinafahamika na kutumika. OCP hutumika kama dawa ya kuzuia utungishaji mimba kwa wanawake ambao hawategemei kupata mtoto. OCP hutumika kwa muda mrefu zaidi na hivyo ni vema kufahamu kuhusu taarifa za sasa kutokana na tafiti kuhusu faida na madhara ya kutumia vidonge hivi.
Tafiti ya kwanza ilifanyika kuangalia ongezeko la uzito kwa mabinti wadogo wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24. Tafiti hii ilifanyika kwa wanawake 138 ambao walichagua kutumia dawa za uzazi wa mpango na 35 walichagua kutumia njia ya kizuizi na wakaangaliwa kwa muda wa miezi 12.
Matokeo;
Kulikuwa hakuna utofauti mkubwa kati ya makundi haya mawili, mabinti watano tu walilipoti kuongezeka uzito katika kundi la waliotumia dawa za OCP ambapo ni sawa na asilimia 3.7
Kulikuwa hakuna utofauti wa mgawanyo wa mafuta mwilini
Tafiti ya pili iliyofanywa na Abbey B.Berenson MD na wengine kuangalia ongezeko la uzito na kubadilika kwa mgawanyo wa mafuta mwilini kutokana na matumizi ya dawa za uzazi wa mpango kwa kipindi cha miaka mitatu tu. Jumla ya wanawake 703 waliingia kwneye tafiti, kati yao wanawake 245 walitumia njia ya vidonge vya majira, wanawake 240 walitumia sindano ya depo(DMPA) na wanawake 218 walitumia njia za vizuizi na kalenda.
Matokeo;
Miaka mitatu ilipotimia waliotumia njia ya sindano ya depo waliongezeka uzito wa kilo 5, ongezeko la mafuta kwa kilo 4.1. asilimia ya ongezeko la mafuta mwilini lilikuwa asilimia 3.4. Ongezeko hili lilikuwa ni kubwa zaidi kuliko wanawake waliotumia vidonge vya majira na njia za vizuizi tu.
Vidonge vya majira vilionekana kutoongeza uzito
Baada ya miezi sita ya kuacha kutumia sindano ya depo uzito ulipungua kwa kilo 0.42 na wale walioacha vidonge vya majia uzito uliongezeka kwa kilo 0.43
Tafiti ya tatu ilifanyika kuangalia ongezeko la uzito kwa wanawake kati ya umri wa miaka 12 hadi 19wanaotumia njia za uzazi wa mpango kwa vidonge vya majira na dawa ya kuchoma ya depo kwa mwaka mmoja wa matumizi.
Tafiti hii iliangalia taarifa zilizorekodiwa tayari kwenye vituo mbalimbali vya afya.
Matokeo;
Kati ya wanawake 239 walioangaliwa 122 walitumia vidonge vya majira na 117 walitumia sindayo ya depo. Waliotumia sindano ya depo wastani wa ongezeko la uzito lilikuwa ni kilo 4 na wale waliotumia dawa za vidonge vya majira waliongezeka kwa kilo 2.
Hitimisho
Kutokana na tafiti hizo tatu zilizofanyika kwa namna tofauti, makala hii inahitimisha kwamba
Vidonge vya majira vinaonekana kusababisha ongezeko la uzito kwa kiasi kidogo sana au kutoongeza uzito kabisa kwa watumiaji
Dawa ya uzazi wa mpango ya depo(DMPA) imeonekana kuhusuana na ongezeko kubwa la uzito kwa watumiaji na kubadilisha mpangilio wa mafuta mwilini
Njia zingine za uzazi wa mpango ambazo hazitumii homoni za progesterone na estrogeni kama kizuizi zinaonekana kutosababisha ongezeko la uzito.
Je unaweza kutumia dawa za uzazi wa mpango kuongeza uzito?
Kutokana tafiti zilizofanyika, endapo unatumia njia ya uzazi wa mpango haswa njia ya sindano ya Depo unauwezekano wa kuongezeka kilo 2 hai 5 kwa mwaka. Hivyo njia hii inaweza kutumika kwa wanawake ambao wanatamani kuongezeka uzito. Hata hivyo faida na madhara ya dawa za uzazi wa mopango zinapaswa kuzingatiwa kabla ya matumizi ya njia hii. Unashauriwa kuwasiliana na daktari wako kwa ushauri zaidi.
Endeleaa kusoma kuhusu njia za uzazi wa mpango na madhara yake kwa kubonyeza hapa
Rejeza za makala hii;
M.D. Sarah Carpenter etal.Weight gain in adolescent and young adult oral contraceptive users. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/3759603/. Imechukuliwa 20.11.2020
SYLVIA L. CEREL-SUHL, M.D.Update on Oral Contraceptive Pills. https://www.aafp.org/afp/1999/1101/p2073.html. Imechukuliwa 20.11.2020
ULY CLINIC. Njia za uzazi wa mpango. https://www.ulyclinic.com/njia-za-uzazi-wa-mpango. Imechukuliwa 20.11.2020
Abma JC, Chandra A, Musher WD, Peterson LS, Piccinino LJ. Fertility, family planning and woman's health: new data from the 1995 national survey of family growth. Vital Health Stat. 23 1997;(19):1–114. Imechukuliwa 20.11.2020
Abbey B.BerensonMD etal. Changes in weight, total fat, percent body fat, and central-to-peripheral fat ratio associated with injectable and oral contraceptive use. https://www.sciencedirect.com/science/article/abs/pii/S0002937808024605. Imechukuliwa 20.11.2020
Sharon AManganMD .Overweight Teens at Increased Risk for Weight Gain While Using Depot Medroxyprogesterone Acetate. https://www.sciencedirect.com/science/article/abs/pii/S1083318801001474. Imechukuliwa 20.11.2020
Comentários