Imeandaliwa na daktari wa ULY-Clinic
Saratani ya damu-Leukemia
​
Utangulizi
​
Leukemia ni saratani ya tishu zinazotengeneza damu. Saratani hizi hutokea kwenye tishu za urojo wa mifupa na mfumo wa limfu.
​
Aina nyingi za saratani ya damu zinajulikana. Baadhi ya saratani hutokea sana kwa watoto na zingine hutokea kwa watu wazima na wazee.
​
Leukemia siku zote huwa ni saratani ya chembe nyeupe za damu. Chembe nyeupe za damu hufanya kazi kubwa ya kupambana na maambukizi yanayoingia mwilini. Kwa kawaida hukua na kuongezeka kwa kujigawa kwa utaratibu maalumu kwa jinsi mwili unavyohitaji idadi Fulani ya chembe hizo.
Kwa mtu mwenye saratani ya hii, ute wa mifupa yake huwa unazalisha chembe hizi zisizo za kawaida na kwa idadi isiyohitajika mwilini na huwa hazifanyi kazi zake vema mara baada ya kuzalishwa.
​
Matibabu ya saratani ya chembe nyeupe za damu huwa ya mlolongo mrefu na hutegemea kwenye aina ya saratani na mambo mengine. Hata hivyo kuna utaratibu na mipango yakufanya ili matibabu yafanikiwe.
Dalili za saratani ya damu
Dalili za saratani ya chembe nyeupe za damu hutegemea aina ya saratani. Dalili zinazotokea kwa wingi ni;
-
Homa na kutetemeka
-
Uchovu endelevu, mwili kuchoka
-
Maambukizi ya mara kwa mara au maambukizi makali
-
Kupoteza uzito
-
Kuvimba tezi limfu/mitoki, kuvimba ini au bandama
-
Kujeruhiwa kirahisi, ama kutoka na damu kirahisi
-
Kujirudia rudia Kutokwa na damu puani
-
Kuwa na wekundu chini ya ngozi-kwa watu wenye ngozi nyeupe
-
Kutokwa na jasho sana wakati wa usiku
-
Maumivu ya mifupa, maumivu mifupa ikishikwa
​
Soma zaidi kuhusu dalili zingine kwa kubonyeza hapa
​
Mwone daktari endapo unapata dalili hizi, kumbuka dalili za saratani ya damu awali huwa zinachanganya sana, mtua anaweza asiwe makini kujua ni tatizo hili kwa sababu huweza kufanana na dalili kama za mafua na magonjwa mengine yatokeayo kwa mtu.
Visababishi
Wanasayansi bado hawajui kisababishi harisi cha saratani ya damu. Inaonekana hutokana na muunganiko wa mambo ya kijeni na mazingira.
Jinsi gani saratani inavyotokea
Kwa ujumla, saratani ya damu hutokea pale endapo chembe zinazotengeneza damu zimepata mabadiliko ya kijeni katika DNA yake- DNA ni kama mwelekezaji ,hutoa taarifa za utengenezaji kazi. Kunawezekana kuna mabadiliko mengine katika chembe hizi ambayo hayaeleweka vizuri ambayo huweza changia katika usababishaji wa saratani ya damu.
Aina Fulani ya udhaifu kwenye chembe za damu huchangia kusababisha uzalishai wa haraka wa chembe za damu na kusababisha ziishi kwa mda mrefu ambapo chembe za kawaida zisingefikisha umri huo. Mda unavyosonga chembe hizi huwa nyingi na hujikusanya kwenye mifumo mbalimbali mwilini ikiwemo kwenye ute wa mifupa na hivyo husababisha kufunika kwa chembe nyeupe zilizo za kawaida na hupelekea upunfufu wa chembe nyeupe za damu, chembe nyekundu za damu na chembe za ugandishaji damu. Kupungua kwa chembe hizo husababisha dalili na viashiria vya ugonjwa huu.
Vihatarishi
Mambo ambayo yanakuongezea hatari ya kupata saratani ya damu ni
Kuwahi kutibiwa saratani
Watu ambao wameshatumia dawa aina Fulani ya kutibu saratani na mionzi huwa na hatari ya kupata saratani zingine ikiwa pamoja na saratani ya damu.
Matatizo ya kijeni
Matatizo ya kijeni yameonekana kuchangia tatizo la kupata saratani ya damu matatizo ya kuzaliwa nayo kama down syndrome, huwa ni kihatarishi cha kupata saratani ya damu
Kutumia kemikali aina Fulani
Kemikali aina ya benzene inayopatikana kwenye mafuta ya gari na hutumika kwenye viwanda vya kemikali huhusianishwa na hatari ya kusababisha saratani ya damu
Uvutaji wa sigara/tumbaku
Kuvuta tumbaku huongeza hatari ya kupata saratani ya AML
Kuwa na historia ya saratani hii kwenye familia
Kama ndugu mmoja kwenye familia amewahi kukutwan a tatizo la saratni ya damu, hatari ya kupata saratani ya damu kwa mtu mwingine huongezeka.
Hata hivyo watu wengi wenye vihatarishi vya kupata sartani huwa hawapati saratni hizo, na wale waliopata pia hawana historia ya kuambatana na vihatarishi tajwa hapo juu.
Mgawanyo wa saratani
Madaktari wameigawa saratani hii kwa kutegemea kasi ya maendeleo ya ugonjwa na aina ya chembe zinazohusika
mgawanyiko wa kwanza ni
Acute leukemia
Aina hii ya Saratani ya damu, chembe za damu huzalishwa na kuachiliwa kwenye damu zikiwa bado hazijakomaa kwa jina huitwa blast. Chembe hizi haziwezi kufanya kazi zake za kulinda mwili, hujizalisha kwa haraka na hivyo ugonjwa huwa mbaya zaidi kwa haraka pia. Saratani ya damu aina hii huhitaji matibabu dhabiti na makali.
Leukemia sugu
Kuna aina nyingi za saratani ya damu iliyo sugu. Baadhi huzalisha chembe nyeupe kwa wingi na zingine huzalisha kwa kiwango kidogo. Saratani sugu huzalisha chembe za ulinzi zinazokaribiana kufanana na chembe za kawaida yaani zilizokomaa, hujizalishwa kwa kasi ndogo na huweza kufanya kazi za kinga ya mwili kwa mda Fulani. Baadhi ya saratani sugu za damu huwa hazionyeshi dalili za awali na wakati mwingine huwa hazitambuliwi kabisa kwa miaka mingi.
Aina ya pili ya mgawanyiko wa saratani ya damu ni kutokana na aina ya chembe nyeupe iliyoathiriwa
Saratani ya damu ya chembe limfu
Hii ni aina ya saratani inayodhuru chembe za limfu ambazo hutengeneza tezi limfu- tezi limfu hutengeneza chembe za limfu ambazo hukaa kwenye mishipa ya limfu-mitoki
Saratani ya damu ya myelogeneous
Aina hii hudhuru chembe za ulinzi aina ya myeloid, chembe za myeloid hutengeneza chembe nyekundu za damu, chembe nyeupe za damu na chembe za kugandisha damu
Kwa hiyo aina za saratani ya damu ni kama vile;
Acute lymphocytic leukemia (ALL)
Huongoza kwa kudhuru watoto wadogo, pia huweza kutokea kwa watu wazima sio sana. Saratani hii hutokea mara nyingi sana kuliko zingine
Acute myelogenous leukemia (AML)
Hutokea mara nyingi, hutokea kwa watoto na watu wazima. Huongoza kuwapata watu wakubwa
Chronic lymohocytic leukemia
Hutokea sana kwa watu wakubwa, mtu hujihisi mzima kwa miaka mingi bila kuhitaji matibabu.
Chronic myelogenous leukemia (CML)
Aina hii hudhuru watu wakubwa pia, mtu hupata dalili kidogo au huwa hana dalili zozote kwa miezi hadi miaka kabla ya kuingia kipindi ambacho chembe zinajizalisha kwa kasi na kuonyesha dalili.
Aina nyingine
​
Aina nyingine zinazotokea kwa nadra ni kama vile Hairly leukemia, myelodysplastic syndrome na myeloproliferative disorders
​
Vipimo na matibabu
Daktari anaweza kujua unatatizo la saratani ya damu akiwa anafanya vipimo vingine tu vya ugonjwa mwingine, yaani kwa baati mbaya kabla hata dalili na viashiria havijaonekana. Vipimo vya msingi vinavyotakiwa/vinavyoweza kufanyika ni;
Uchunguzi wa mwili
Ataangalia viashiria vinavyoonekana, viashiria vya kuishiwa damu, kuvimbakwa mitoki au tezi limfu ini na bandama.
Vipimo vya damu
Kwa kipimo cha kuangalia damu yako, daktari anaweza kutambua kama una kiwango kisicho cha kawaida cha chembe nyeupe ama chembe za kugandisha damu na hivo kutambua ni aina gani ya saratani ya damu uliyonayo.
Kipimo cha mifupa
Ute ute kwenye mifupa huweza kuchukuliwa na kupimwa maabara hasa kutoka kwenye fupa nyonga. Ute ute huo hupelekwa kwenye vipimo na kuangaliwa sifa za chembe zinazozalisha damu.
Unaweza kupimwa vipimo vingine pia kuangalia ukubwa wa tatizo ama kufanya uchaguzi wa matibabu yako
​
ULY clinic inaksuhauri kuwasiliana na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile inayohusu afya yako.
​
​
​
Imeboreshwa mara ya mwisho, 2.09.202020
​
Rejea za mada hii,
​
-
Davidson's Essentials of Medicine edited by J.Alaslair Innes Ukurasa wa 547-552
-
2. Long Cases in Clinical Medicine kimeandikwa na ABM Abdullah kurasa wa 633-638
-
Imechukuliwa 02.07.2020http://www.cancer.gov/publications/patient-education/wyntk-leukemia.3. What you need to know about leukemia. National Cancer Institute.
-
2.07.2020 Imechukuliwa http://www.lls.org/resourcecenter/freeeducationmaterials/leukemia/understandingleukemia.4. Leukemia. Leukemia & Lymphoma Society.
-
Taking time: Support for people with cancer. National Cancer Institute. http://www.cancer.gov/publications/patient-education/taking-time. Imechukuliwa 2.07.2020