Imeandikwa na Daktari wa ULY CLINIC
Jumanne, 28 Aprili 2020
Adreno
Tezi za adreno ni jozi ya tezi mbili zilizopo juu ya kila figo. Tezi hizi zina umbo la piramidi. Kwa mtu mzima tezi moja inaweza kuwa na urefu wa sentimita 3 hadi 5, upana wa sentimita 2 hadi 3 na unene wa sentimita 1, huku uzito wa tezi moja unaweza kuwa gramu 3.5 hadi 5.
Tezi hizi zina matabaka mawili;
• Tabaka la nje (Adreno koteksi na
• Tabaka la ndani (adreno medula)
Maelezo ya ziada yanapatikana hapa chini kuhusu
Tabaka la nje ( adreno koteksi )
Tabaka hili linatoa homoni ambazo zipo kwenye makundi matatu ambayo ni;
1. Homoni zinazohusika na kurekebisha kiwango cha madini ya sodiamu na potashiamu kwenye damu. Homoni ya muhimu kwenye kundi hili ni aldosterone.
Kwa kurebisha kiwango cha madini haya, aldostrone inamahakikisha shinikizo la damu (presha ya damu) linabaki kwenye kiwango cha kawaida.
2. Homoni zinazo rekebisha uchakataji wa wanga, mafuta na protini ili kuzalisha nishati mwilini (glucocorticoids)
Homoni hizi ni;
• Haidrokotisoni- Hii hutolewa zaidi ya zingine.
• Kotikosterone
• Kortisone
Kazi za homoni hizi ni;
• Kuchochea ubadilishaji wa glaikojeni kuwa glukosi ili kuzalisha nishati ya mwili.
• Kubadili protini na mafuta kuwa glukosi (glucose) ili kuzalisha nishati.
• Kuchochea protini kutumika kuzalisha nishati.
• Kuchochea mafuta kutumika kuzalisha nishati.
• Pia homoni hizi zina uwezo wa kushusha kinga ya mwili (Kazi za anti inflamatori).
3. Homoni za kike na za kiume: Homoni hizi hutolewa kwa kiasi kiasi kidogo ukulinganisha na zinatolewa kutoka kwenye korodani na ovari baada ya mtu kubalehe.
Tabaka la ndani (adreno medula)
Tabaka hili linatoa homoni mbili ambazo ni adrenaline na noradrenaline.
Homoni hizi hutolewa wa wakati mwili unajaribu kukabiliana na hatari inayohitaji utatuzi wa haraka kama vile kukimbia, kupigana au vinginevyo.
Homoni hizi hufanya yafuatayo;
• Kuchochea ongezeko la kasi ya mapigo ya moyo.
• Kuchochea ongezeko la shinikizo la damu (presha).
• Kuelekeza damu katika viungo muhiumu kama vile ubongo, moyo,misuli na kupunguza damu maeneo mengine yasiyo na umuhimu wakati wa hatari.
• Kuchochea kuongeza ufanyaji kazi wa mwili mzima.
• Kusababisha mboni za macho kutanuka zaidi kuruhusu kuona vizuri zaidi.
Dosari za tezi za adrenali
Tezi za adrenari zinaweza kupata dosari mbalimbali na mtu ataonesha dalili kulingana na dosari husika.
Dosari yoyote itasababisha tezi kutoa homoni nyingi kupita kiasi au kidogo chini ya kiasi kinacho hitajika, hivyo kusababisha hitilafu mwilini.
Miongoni mwa dosari hizo, za muhimu ni pamoja na;
• Uvimbe kwenye tezi ya adrenali.
• Saratani ya tabaka la nje la tezi ya adrenali (Saratani ya adrenalkortiko).
• Sindromu ya kushing
• Uvimbe kwenye tabaka la ndani la tezi ya adrenali (pheochromocytoma).
• Ugonjwa wa kuzaliwa wa haipaplezia ya adreno
• Uvimbe kwenye tezi ya pituitari.
• Ugonjwa wa Addison’s
• Tezi ya adrenali kutoa homoni ya aldosteroni nyingi kupita kiasi (hypaaldosteronizimu).
Dalili za tezi ya adreno yenye dosari
Dalili ya dosari ya tezi za adreno hutegemea kisababishi, miongoni mwa dalili hizo ni;
• Shinikizo la juu la damu (presha ya kupanda)
• Mapigo ya moyo kwenda kasi kuliko kawaida
• Uzito mkubwa kupita kiasi.
• Mwanamke kuwa na maumbile au muonekano wa kiume.
• Kuwai kubalehe.
• Kuumwa kichwa.
• Kuchoka sana kuliko kawaida.
Dalili zaidi ya ziilizotajwa hapo juu zinaweza kuwepo kutegemeana na dosari husika kwenye tezi za adrenali.
Wasiliana na daktari wako endapo umeona kuwa una dalili yoyote ile katika maelezo haya kwa ushauri na tiba
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba zaidi kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii au kubonyeza hapa.
Imeboreshwa,
13 Julai 2021, 18:28:47
Rejea za mada hii;