top of page

Imeandikwa na Daktari wa ULY CLINIC

Jumapili, 26 Aprili 2020

Haipothalamasi

Haipothalamasi

Haipothalamas (hypothalamus) ni sehemu ndogo ya ubongo yenye kazi muhimu katika mfumo ya fahamu na homoni. Sehemu hii ina kazi kubwa ya kuhakikisha kazi mbalimbali za mwili zinafanyika kwa usahihi na mtu anakua mwenye afya pasipo mapungufu. Sehemu hii ya ubongo inaweza ikawa na uzito unaoweza kufika gramu 7 kwa mtu mzima.

Kazi za tezi ya haipothalamasi

• Kutoa homoni: Homoni hizi huchochea au kuzuia tezi ya pituitari kutoa homoni ambazo nazo huchoche tezi nyingine mwilini kutoa homoni zake.
• Kurekebisha hisia za mtu kulingana na mazingira: mfano hisia za furaha, huzuni,woga n.k.
• Kurekebisha hamu ya kula na kunywa.
• Kurekebisha joto la mwili.
• Kurekebisha mzunguko wa kulala na kuamka.
• Kurekebisha kazi za mfumo wa fahamu wa matendo yote yasiyo ya hiari. Mfano mapigo ya moyo, mmeng'enyo wa chakula, n.k
• Kuwezesha utofauti wa tabia za kiume na zakike.
• Kurekebisha kiwango cha maji mwilini na kiu.

Homoni zinazotolewa na haipothalamasi

Miongoni mwa kazi za haipothalamasi ni kutoa homoni. Haipothalamasi huzalisha homoni ambazo huingia kwenye tezi ya pituitari kupitia mishipa ya damu. Homoni hizi zipo za aina mbili;

• Homoni zinazo chochea tezi ya pituitari kutoa/kuzalisha homoni na
• Homoni zinazo pinga tezi ya pituitari kuzalisha homoni nyingine ambazo nazo huenda kuchochea tezi nyingine mwilini kutoa homoni zake

Homoni hizi ni;

• Growth hormone releasing hormone (RHRH)
• Growth hormone release inhibiting hormone (GHRIH)
• Thyrotropin releasing hormone (TRH)
• Corticotrophin releasing hormone (CRH)
• Prolactin releasing hormone (PRH)
• Prolactin inhibiting hormone (PIH)
• Luteinizing hormone releasing hormone (LHRH)
• Gonadotrophin releasing hormone (GnRH)

Kila homoni imeelezewa kwa undani sehemu ndani ya tovuti hii. Tafuta homoni unayotaka kusoma kwenye kiboksi cha “Tafuta chochote unachokitaka hapa…”

Dosari za tezi haipothalamasi

Dosari kwenye haipothalamasi hudhihirika kwa dalili zifuatazo;

• Joto la mwili kubadilika badilika
• Kudumaa (Umbo la ufupi usio wa kawaida)
• Kukojoa sana kupita kiasi
• Kukosa hamu ya kula
• Kukosa usingizi
• Utasa
• Kuchelewa kubalehe
• Uzito mdogo au mkubwa kupita kiasi
• Shinikizo la damu la juu au chini.

Visababishi vya dosari kwenye tezi ya haipothalamasi

• Kasoro za kuzaliwa kwenye vinasaba(DNA)
• Kasoro za kuzaliwa kwenye ubongo
• Uvimbe kwenye ubongo
• Majeraha ya kichwa
• Upasuaji wa ubongo
• Upungufu wa lishe

Wasiliana na daktari wako endapo umeona kuwa una dalili yoyote ile katika maelezo haya kwa ushauri na tiba

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba zaidi kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii au kubonyeza hapa.

Imeboreshwa,

13 Julai 2021, 18:37:22

Rejea za mada hii;

1.Principles of anatomy and physiology Toleo la 12 ISBN 978-0-470-08471-7 by Gerard J. Tortora and Bryan Derrickson ukurasa wa 512 na 650

2.Ross and Wilson Anatomy and Physiology in healthy and illness 12th Edition ISBN 978-0-7020-5325-2 ukurasa wa 159 na 219

3.Healthline: https://www.healthline.com/human-body-maps/hypothalamus imechukuliwa 25/04/2020.

4.Madescape: https://emedicine.medscape.com/article/1949061-overview#showall imechuliwa 25/04/2020.
bottom of page