top of page

Mwandishi:

Dkt. Mangwella S, M.D

Mhariri:

Dkt. Adolf S, M.D

Jumatatu, 24 Julai 2023

Mimba ya miezi miwili

Mimba ya miezi miwili

Mimba ya miezi miwili humaanisha mimba ya wiki 4 hadi 8. Katika makala hii utajifunza nini kinatokea kwenye mimba ya wiki 5 hadi 8 za ujauzito.


Mimba ya wiki 5

Utakosa hedhi yako na endapo utapima kipimo cha ujauzito utakutwa na mimba. Utaanza kupata dalili za ujauzito ambazo ni;


  • Maumivu ya titi

  • Uchovu

  • Kichefuchefu

  • Tumbo kujaa gesi

  • Kukojoa mara kwa mara



Mabadiliko kwa kijusi

Ogani kuu za mwili wa mtoto huanza kutengenezwa ikiwa pamoja na;

  • Moyo

  • Ini

  • Figo

  • Mapafu

  • Ubongo


Mtoto huwa na ukubwa wa sentimita 0.25 wakati huu na hufanana na kiluwiluwi. Nje ya mwili wa kiluwiluwi huonekana michomozo mine ambayo itakuwa mikono na miguu ya mwanao.


Mambo mengine ya kufahamu

Katika hatua hii, mtu hawezi kusema kuwa una ujauzito kwa kukuangalia mwonekano wa nje licha ya kutokea kwa mabadiliko makubwa ndani ya mwili.


Mimba ya wiki 6


Kuwa na hisia za juu au chini hutokea sana kipindi hiki. Mabadiliko ya hisia hutokea kutokana na mabadiliko ya homon yanayoendelea mwilini mwako wakati mtoto anaendelea kukua.


Ukiweka kando mabadiliko ya homon kando, unaweza kuwa na mabadiliko ya hisia kutokana na mawazo ya hali yako ya ujauzito tu.


Unapaswa kuhudhuria kliniki mara ya kwanza ili kuonana na daktari au mhudumu wa afya kwa ushauri. Mara utakapofika utafanyiwa kipimo cha ultrasound ili kutoa mwangaza wa kijusi tumboni. Kufanya kipimo hiki pia husaidia kuwa na majibu mazuri ya kuliganisha ukuaji wa mtoto na tarehe ya kujifungua.


Mabadiliko kwa kijusi

Mapigo ya moyo ya mtoto huwa kati ya mapigo 100 hadi 160 kwa dakika.


Nini unatakiwa kufanya?
  • Hupaswi kuwa na hofu endapo utaona unatokwa na matone kidogo ya damu wakati huu haswa kama hayaambatani na maumivu ya tumbo au kubana kwa tumbo la chini

  • Kutokwa na matone kiasi ya damu ukeni ni hali ya kawaida kama damu inayotoka ni kidogo na inaataka kufanana na damu ya hedhi lakini, huwa na rangi nyekundu au kahawia.

  • Hata hivyo ukitokwa na damu unapaswa kuwasiliana na daktari kwa ushauri kwa kuwa hali hii inaweza kuashiria pia dalili ya mimba inayotishia kutoka au ujauzito uliotungwa nje ya kizazi. Kutungwa kwa ujauzito nje ya kizazi hutishia uhai wa mama hivyo hutakiwa kudhibitiwa mapema.


Viungo vya mtoto

Wakati huu viungo vya nje ya mwili huanza kuonekana kama vile;

  • Pua

  • Midomo

  • Masikio


Mengine unayopaswa kufahamu

Mtoto huanza kucheza tumboni, kwa vile huwa mdogo sana, hutaweza kupata hisia za mtoto kucheza.


Mimba ya wiki 7


Nini kinatokea ndani ya mwili wako?

  • Mfuko wa kizazi huongezeka mara mbili ya kawaida yake ndani ya wiki tano zilizopita.

  • Unaweza kupata shida ya kula kutokana na hisia za kichefuchefu.

Wiki ya 7 ya ujauzito

  • Unaweza kupata tabia pia ya kutaka kula vyakula aina fulani tu, hata vile ambavyo awali ulikuwa huvipendi. Hali hii ni kawaida kutokea na unapaswa kuhakikisha kuwa unakula mlo kamili.

  • Badiliko kubwa jingine linalotokea mwilini mwako wiki ya 7 ya ujauzito ni kuanza kutengenezwa kwa kizibo cha mdomo wa shingo ya kizazi. Kizibo hiki hutengenezwa na ute mzito unaotoka kwenye shingo ya kizazi ili kuzuia vimelea vya marashi pamoja na vitun vingine vilivyomo nje ya mwili kuingia ndani ya kizazi. Ute huu huondoka wakati wa uchungu wa kujifungua.


Mabadiliko yanayotokea kwa mtoto tumboni
  • Mwanao tumboni huanza kupata mwonekano wa mtu. Huwa na viganga vidogo na kanyagio na huanza kukua. Mkia wa kijusi pia huanza kupungua urefu.

  • Mwanao wakati huu huwa na urefu wa sentimita 1.25 sawa na ukubwa wa punje ya mbaazi.

  • Kongosho na kidole tumbo pia huwa imeshatengenezwa tayari kusaidia mmen’enyo wa chakula.


Mambo unayotakiwa kuzingatia
  • Wakati huu tegemea kukojoa mara kwa mara kutokana na ongezeko la maji mwilini mwako.

  • Utaongezeka uzito pia kutokana na ongezeko la maji mwilini.

  • Unapaswa kukojoa mara nyingi iwezekanavyo kwa kuwa kuzuia mkojo sio afya kwa kibofu chako.


Mimba ya wiki 8

Hii ni wiki ya mwisho katika mimba iayokamilisha mwezi mmoja (1) wa ujauzito.


Nini hutokea mwilini mwako kwenye wiki ya 8 ya ujauzito?

  • Kiwango kikubwa cha homon mwilini mwako huamsha ukuaji wa matiti ili kukuandaa kwa ajili ya kunyonyesha mtoto.

Wiki ya 9 ya ujauzito

  • Matiti yako yanaweza kuendelea kukua umbile na ukubwa katika kipindi chote cha ujauzito na utapaswa kujiandaa kupata brazia inayoweza kutosheleza matiti yako

  • Ongezeko kubwa la homon progesterone huweza pelekea hisia za uchovu, kichefuchefu na kutapika.

  • Tabia ya kulala inaweza kubadilika kutokana na kukojoa mara kwa mara na unaweza kujihisi vibaya.


Nini kinatokea kwa mtoto tumboni?
  • Mwanao tumboni huanza kupata mwonekano wa binadamu wakati kope za macho zinapoanza kutengenezwa. Mapafu na ubongo wa mtoto hukua zaidi.

  • Ubongo huanza kutengeneza chembe za neva ambazo huungana na nyingine na kutengeneza njia za awali za mishipa ya kale ya mfumo wa fahamu.


Mambo unayotakiwa kuzingatia

Wakati huu kwa kuwa mwili unaendelea kuongezeka, nguo zitaanza kukubana na hivyo utatakiwa kununua nguo kubwa zinazoacha mwili wako huru.


Majina mengine ya makala hii

MImba ya miezi miwili (2) huwa na maana pia ya

  • Ujauzito wa miezi miwili

  • Ujauzito wa miezi 2

  • Mimba ya wiki 5 hadi 8

Imeboreshwa:

Jumatatu, 24 Julai 2023 20:20:47 UTC

Rejea za mada hii:

  1. American Society for Reproductive Medicine; American College of Obstetricians and Gynecologists' Committee on Gynecologic Practice. Prepregnancy counseling: Committee Opinion No. 762. Fertil Steril. 2019 Jan;111(1):32-42. [PubMed]

  2. Berglund A, et al. Preconception health and care (PHC)-a strategy for improved maternal and child health. Ups J Med Sci. 2016 Nov;121(4):216-221. [PMC free article] [PubMed]

  3. Annadurai K, et al. Preconception care: A pragmatic approach for planned pregnancy. J Res Med Sci. 2017;22:26. [PMC free article] [PubMed]

  4. McClatchey T, et al. Missed opportunities: unidentified genetic risk factors in prenatal care. Prenat Diagn. 2018 Jan;38(1):75-79. [PubMed]

  5. Ko SC, et al. Estimated Annual Perinatal Hepatitis B Virus Infections in the United States, 2000-2009. J Pediatric Infect Dis Soc. 2016 Jun;5(2):114-21. [PubMed]

  6. Tohme RA, et al. Hepatitis B virus infection among pregnant women in Haiti: A cross-sectional serosurvey. J Clin Virol. 2016 Mar;76:66-71. [PMC free article] [PubMed]

  7. Bhavadharini B, et al. Screening and diagnosis of gestational diabetes mellitus - relevance to low and middle income countries. Clin Diabetes Endocrinol. 2016;2:13. [PMC free article] [PubMed]

  8. ACOG Practice Bulletin No. 190 Summary: Gestational Diabetes Mellitus. Obstet Gynecol. 2018 Feb;131(2):406-408. [PubMed]

  9. Rule T, et al. Introducing a new collaborative prenatal clinic model. Int J Gynaecol Obstet. 2019 Mar;144(3):248-251. [PubMed]

bottom of page