Imeandikwa na ULY CLINIC
​
Viashiria vya Uhai
​
Viashiria uhai ni viashiria vinavyoonyesha uhai wa mwili au hali ya utendaji kazi wa mwili. Viashiria uhai vinavyopimwa sana hospitali ni vinne, ambavyo ni;
-
Joto la mwili
-
Kiwango cha capigo ya moyo
-
Kiwango cha mapigo ya upumuaji
-
Kiwango cha shinikizo la damu
​
Viashiria hivi huonyesha hali ya uzima wa mtu na kwa namna gani mwili unavyofanya kazi kuitikia dhidi ya hali na magonjwa mbalimbali. Kwa kawaida vishiria uhai hutakiwa kupimwa na kurekodiwa kwa rejea ya hapo baadae.
Ni wakati gani viashiria vya uhai vinatakiwa kupimwa?
Viashiria uhai mara nyingi hupimwa hospitali kwa wagonjwa wote wanaoumwa, kifaa tiba maalumu kinachoitwa ECG 'monior' hupima viashiria vyote kwa pamoja. Endapo umewahi kuingia ICU utaona mashine ambayo inatoa sauti kwa mwendelezo wakati huo kuna kioo kinachoonyesha namba zinazobadilika kila sekunde, mashine hii itakuwa na waya ambazo zimeshikizwa kwenye mwili wa mgonjwa. Hii huwasaidia wataalamu wa afya kuangalia maendeleo ya matibabu na utendaji kazi wa mwili wa mgonjwa
Hata hivyo kila mtu anatakiwa kufahamu kuhusu viashiria uhai vyake vikoje angalau kila mwezi, hii itasaidia kumpa mwangaza daktari wako endapo mabadiliko yametokea wakati hali ya mwili wako imebadilika au unaumwa. Utatakiwa kujipima wewe au na mtu mwingine ambaye anafahamu kupima ukiwa nyumbani.
Kwa watu wanaofanya mazoezi ya mwili, ni vema sana kujipima uimara wa mwili wako kwa kutumia viashiria vya uhai, vipimo hivi huweza kukusaidia kufikia malengo fulani mazuri kiafya.
Makala hii imezungumzia kiundani namna ya kupima viashiria vya uhai ukiwa nyumbani kwako
Vifaa gani vinatakiwa wakati wa kupima viashiria vya uhai?
Vifaa unavyotakiwa kuwa navyo ni
Kipimajoto
Unaweza kutumia kipima joto cha kidigitali au cha kianalogia. Kipima joto cha kianalogia ni kizuri zaidi endapo unaweza kukitumia na kukisoma vema. Kipimajoto cha kidigitali ni rahisi kukitumia hata hivyo endapo betri zimeisha au hazina nguvu, majibu yatakayotolewa na kipimo huwa si sahihi.
Kuna aina nyingi za vipimajoto vya kidigitali, aina nyingine ni nzuri kutumika kwa watoto na zingine kwa watu wazima.
Kipima shinikizo la damu
Kifaa hiki huitwa kwa jina jingine la kilatini kama sphygmomanometer, kuna aina mbili pia za kipimo hiki, kipimo cha kidigitali na kipimo cha kianalogia. Kama ilivyo kawaida kipimo cha kidigitali ambacho kinatumia betri huweza kusoma majibu yasiyo sahihi (isipokuwa kinachotumia umeme wa moja kwa moja kwenye chanzo yaani soketi) endapo betri imeishiwa nguvu hata hivyo huwa ni rahisi kukitumia na hutoa majibu haraka kwani hakihitaji utaalamu kama kipimo cha analogia. ULY CLINIC inashauri endapo unatumia kipimo cha kidigitali, tumia betri mpya na baada ya kuzitumia zitoe kwenye kufaa chako, endapo utatumia kipimo cha analogia hakikisha unajifunza vema ili kuepuka kupata majibu yasiyo sahihi.
Saa ya mshale au yenye uwezo wa kuhesabu sekunde
Saa ya mshale ni muhimu sana kwenye upimaji wa mdundo wa mapigo ya moyo na mishipa ya damu pamoja na mapigo ya upumuaji. Saa inayotakiwa ni ile ya kutumia mshale au ile inayoweza kuhesabu sekunde.
​Kuendelea kusoma bofya unachotaka kusoma kwenye linki zilizo hapo chini.
​
​​
Imeboreshwa, 06.10.2024
​
Rejea mada:
​
-
John Hopkins medicine. Vital Signs (Body Temperature, Pulse Rate, Respiration Rate, Blood Pressure). https://www.hopkinsmedicine.org/health/conditions-and-diseases/vital-signs-body-temperature-pulse-rate-respiration-rate-blood-pressure. Imechukuliwa 31.12.2020
-
CDC. VItal Signs. https://www.cdc.gov/vitalsigns/index.html. Imechukuliwa 31.12.2020
-
Vitals signs in children. https://www.mottchildren.org/health-library/abo2987. Imechukuliwa 31.12.2020