top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

Jumatatu, 14 Agosti 2023

Mbinu za kufanya mtoto anywe dawa

Mbinu za kufanya mtoto anywe dawa

Inapokuja suala la kumpa mtoto dawa ni jambo linaloumiza vichwa wazazi wengi. Hata kama dawa ni tamu, mara mtoto anapotambua tu kuwa anachopewa ni dawa huanza kulia na kama ukifanikiwa kumpa atajitapisha kwa kuwa mwili wake umeshaona alichopewa si rafiki. Hii ni moja ya njia ya mtoto kuhakikisha kuwa anachokula kipo salama.


Je unatumia mbinu gani kufanya mtoto anywe dawa?

Kama mzazi au mlezi wa mtoto mdogo, unapaswa kujifunza mambo mengi kwa mtoto ambayo yatakusaidia ufanikiwe kumnywesha dawa pasipo kukataa. Mara nyingi watoto hujifunza mambo mengi kutoka kwa wazazi au watu wanaomzunguka na kufanya uchunguzi na kujaribu kama wanaweza kufanya kile wanachokiona.


Mfano endapo mtoto chini ya mwaka mmoja ataona unakula chakula, hata kama ni kikali, au kichungu, naye atapenda aonje na kuendelea kula vile vile kwa sababu mzazi unafanya hivyo. Hivyo hivyo unaweza kutumia saikolojia hii kumfanya mtoto anywe au ale dawa au chakula. Zifuatazo ni baadhi ya njia unazoweza kutumia:

  1. Kuigiza unatumia dawa hiyo

  2. Kutumia chombo tofauti cha kumnyweshea dawa

  3. Kuchanganya dawa na chakula

  4. Kubadilisha njia ya kumpa dawa


Kuigiza unatumia kile unachompa

Njia hii humfanya mtoto aone anachopewa ni kitu kizuri na salama. Unachopaswa kufanya ni kumrubuni kama unakunywa kwanza na kumpa naye atumie.


Kutumia chombo tofauti cha kumnyweshea dawa.

Njia hii hutumiwa sana na huwa na matokeo mazuri. Mambo ya kuzingatia kwenye njia hii ni kubadili chombo ulichozoea kukitumia wakati unampa dawa siku za nyuma, mfano badala ya kutumia kifuniko cha dawa au kijiko, tumia chuchu ya maziwa au kiziba mdomo(pacifier) kinachoruhusu kuweka dawa au chombo chochote ambacho hajazoea kukitumia kwa dawa. Hakikisha unaweka dawa kwenye chombo hicho mbali naye ili asione unachokifanya. Unaweza pia kutumia boksi tupu la juisi, n.k ili kumfanya anywe dawa.


Kuchanganya dawa na chakula

Kuna baadhi ya dawa ambazo zinaweza kuchanganywa na chakula hivyo kumfanya mtoto atumie dawa pasipo yeye kufahamu. 

Mumfanya mtoto anywe dawa

Kwa mtoto anapenda sharubati au juisi, unaweza kutumia kopo la juisi ukalifungua mbele yake na kumpa anywe. Hakikisha unaweka dawa kwenye kpo la juisi kicha kulifunga mbali na upeo wa macho yake kabla ya kuliufungua mbele yake na kumpa. Na kama unataka kumpa juisi halisi ya matunda, tia dawa kwanza kwenye bilauri mbali na upeo wa macho yake kisha unapokuwa kweny upeo wake wa macho mimina juisi kidogo akiwa anaona na kumpa na alnywa unaweza muongezea nyingine. Ili kufanya njia hii iwe na mafanikio mimina juisi kwenye glasi yako pia kwenye ili kumsindikiza wakati naye anakunywa glasi yake yenye dawa bila kufahamu.


Mambo ya kuzingatia ni kuhakikisha kuwa kiwango cha chakula unachowekewa akimalize ili atumie dozi ya dawa anayotakiwa kutumia kwa wakati huo.


Pia unapaswa kufahamu kuwa baadhi ya dawa huwa hazitumiki na chakula au chakula aina fulani tu, hivyo kabla ya kutumia njia hii soma mashariti ya dawa husika kama inaruhusiwa kutumika na chakula au la ili kuepuka kupnguza uwezo wa dawa kufanya kazi au kutengeneza mchanganyiko ambao si salama kwa mtoto.


Kubadilisha njia ya kutoa dawa

Kwa dawa ambazo zinatumika kwa kunywa, baadhi yake zinaweza kutumika kwa kuwekwa puruni ( ndani ya njia ya haja kubwa) dawa hizi zinaweza kufyonzwa vema na kufanya kazi. Mambo muhimu ya kuzingatia ni kwamba njia hii inapaswa kutumika kwa mtoto asiye harisha kwa kuwa ili dawa isitolewa kabla ya kufyonzwa. Pia zingatia kuwa baadhi ya dawa zinahitaji kumeng’enywa na tindikali katika tumbo ili zinapoingia kwenye damu ziweze kufanya kazi vema. Hivyo utahitaji ushauri wa daktari pia kama dawa inaweze kutumika kwa kwa njia hii au la.


Wakati wa kuweka dawa kwenye puru, unaweza kutumia bomba la sindano ili kuingiza dawa vema. Hakikisha mtoto  amelala kifudifudi ili asione unachokifanya (njia hii ni nzuri kutumika kwa watoto waliolegea na wasioweza kula)


Kama mtoto anapenda kunyonya vidole unaweza pia kutumia njia hii kumdanganya. Cha kufanya ni kuweka dawa katika chombo nje ya upeo wa macho yake, kisha baada ya kusafisha mikono yako na maji safi, chovya kidole katika dawa na kumpa alambe. Unaweza kuigiza kulamba kidole kisicho na dawa ili kumwonesha kuwa nawewe unafanya hivyo, pia kama mikono yake ni misafi unaweza mpa naye alambe. Hakikisha unachovya na kumlambisha mpaka dawa yote inaisha taratibu.


Kumbuka

  • Unashauriwa kuwasiliana na daktari wako kabla ya kumpa mtoto dawa yoyote ile kwa usalama wake. Mtaalamu wa afya anaweza kukusaidia kumpa mtoto dozi kamili kulingana na uzito na umri wake. 

  • Unapaswa kupima dozi ya dawa kwa kutumia chombo kile kile ambacho umepewa na mtaalamu wa afya ili kuhakikisha kuwa anapata dozi sahihi.

  • Katika kutumia njia zote hizi, haupaswi kuwa na haraka ya kumpa dawa, mpe taratibu ili isiwe ugomvi na kuona anachopewa ni kibaya.


Mambo mengine ya kuzingatia

  • Wasiliana na daktari kabla ya kuvunja au kusaga dawa au kuchanganya na chakula kama vile vyakula vya wanyama wa baharini, barafu, nyama, mboga za majani n.k.

  • Changanya dawa na chakula kidogo ili kuondoa ladha ya dawa na kuifanya iwe na ladha nzuri. Hii husaidia kuficha ladha ya dawa kwa mtoto, kuchanganya na kiasi kidogo cha kitu kitamu pia huweza kusaidia.

  • Baadhi ya dawa zinaweza kuongezewa kiasi kidogo cha chakula, sharubati au maji. Changanya kwa kiasi kidogo kama kijiko kimoja au viwili vya chakula au sharubati au maji yaliyotiwa sukari.

  • Kama mtoto hapendi ladha ya dawa, mpatie kitu kitamu kabla ya kumpa ili kupoteza ladha mbaya, pipi huzubaza tezi za ladha za ulimi na hivyo kufanya asihisi ladha ya dawa.

  • Kama mtoto ni mkubwa, mweleze umuhimu wa kunywa dawa ili aelewe kwanini unampa na kwa ajili ya nini. Mfano dawa hii itasaidia kuondoa maumivu yako ya tumbo.

  • Ikiwezekana chagua namna gani utampa dawa mfano kwa kumpa mwenyewe ashike kijiko, sindano au kikombe kunywa badala ya kumlazimisha.

  • Mpongeze mtoto mkubwa kama akiweza kumeza dawa kwa maneno au hata kumpa zawadi kama stika, kumruhusu akacheze n,k

  • Usimpatie dawa mara baada ya kumwadhibu mtoto. Huweza kufikiria dawa ni sehemu ya adhabu

  • Usimtishie mtoto au kumpiga kama asipokunywa dawa.

  • Mpatie maji baada ya kunywa dawa.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

1 Agosti 2024, 18:33:02

Rejea za mada hii:

Rathi R, Sanshita, Kumar A, Vishvakarma V, Huanbutta K, Singh I, Sangnim T. Advancements in Rectal Drug Delivery Systems: Clinical Trials, and Patents Perspective. Pharmaceutics. 2022 Oct 17;14(10):2210. doi: 10.3390/pharmaceutics14102210. PMID: 36297645; PMCID: PMC9609333.

Hua S. Physiological and Pharmaceutical Considerations for Rectal Drug Formulations. Front Pharmacol. 2019 Oct 16;10:1196. doi: 10.3389/fphar.2019.01196. PMID: 31680970; PMCID: PMC6805701.

https://www.nationwidechildrens.org/family-resources-education/health-wellness-and-safety-resources/helping-hands/medicine-how-to-give-by-mouth#. Imechukuliwa 14.08.2023

bottom of page