top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Jumapili, 20 Oktoba 2024

Ukweli kuhusu mzunguko wa hedhi wa siku 28

Ukweli kuhusu mzunguko wa hedhi wa siku 28

Wanawake wengi wamejifunza vibaya kuwa mzunguko wa hedhi wa kawaida ni siku 28 hivyo unapokuwa tofauti na huyo huwa na wasiwasi na hofu ya kuwa si kawaida.


Mzunguko wa hedhi unaweza kutofautiana kati ya mzunguko mmoja na mwingine na baina ya mwanamke mmoja na mwingine.


Tafiti zilizofanyika kwa wanawake 600,000 zimeonyesha kuwa wanawake 65 kati ya 100 huwa na mzunguko wa hedhi wa kati ya siku 25 hadi 30 na wanawake 13 tu kati ya 100 huingia hedhi ya siku 28.


Idadi hiyo inamaanisha kuwa ni wanawake wachache sana huwa na mzunguko wa hedhi wa siku 28.


Majibu ya tafiti hii yanabidi kukutoa hofu na kukupa ukweli ya kuwa mzunguko wako wa hedhi ni wa kawaida endapo upo ndani ya siku 21 hadi 32. Hauna haja ya kutafuta matibabu kama utakuwa ndani ya siku hizo.


Je, ni kawaida kuwa na mzunguko wa hedhi wa nje ya siku 21 hadi 32?

Ndio, kila binadamu ameumbwa kwa utofauti na ana mwitikio wa utofauti, hii ndio maana tafiti zinaonyesha kuwa kuona ndani ya siku 21 hadi 32 ni wastani tu, huenda endapo tafiti zingefanyika kwa watu wote duniani, wanawake wengi wanaoenda nje ya muda huu wangetambulika. Jambo la msingi kuzingatia ni kama kuna tatizo jingine la kiafya linalosababisha kuchelewa au kuwahi kwa mzunguko wa hedhi. Endapo uchunguzi umedanyika na hakuna tatizo lolote ama dalili zozote za ugonjwa katika mwili, ondoa hofu na amini kuwa mzunguko wako wa hedhi ni wa kawaida hata ukiwa nje ya muda huo.


Ukweli huu una madhara gani?

Kufahamu kuwa mzunguko wa hedhi huwa si wa siku 28 kwa wanawake wengi na kwamba huwa unabadilika badilika kati ya mwezi hadi mwezi hii inatoa sababu ya kwamba, wanawake wengi pia hawawezi kushika ujauzito katika siku za hatari ambazo zinaendana na siku 28 kama ilivyozoeleka.


Inashauriwa endapo unataka kushika ujauzito, shiriki ngono bila kinga bila kujali ni siku ya hatari au la ili kwendana na mabadiliko ya mzunguko wa hedhi ambayo huweza kutokea kila mwezi.


Madhara mengine ni kuhusu tarehe ya kujifungua ambayo mahesabu yake huzingatia idadi ya siku katika mzunguko wa hedhi, wataalamu wengi na wagonjwa huwa wanatumia mzunguko wa siku 28 kama rejea badala ya kutafuta wastani wa siku katika mzunguko wa hedhi kwa kusoma mzunguko wa mama kwa angalau miezi mitatu iliyopita.


Ushauri wa kufahamu idadi ya siku katika mzunguko wako wa hedhi

Ili kufahamu idadi ya siku katika mzunguko wako wa hedhi unapasa kutumia kalenda yako ya kila mwezi, chora duara siku ya kwanza unapoanza kuona hedhi moja na mara utakapoanza kuona hedhi inayofuata na endelea mpaka utakapofikisha miezi angalau mitatu. Wastani wa miezi utakayochora utakuwa wastani wa siku katika mzunguko wako wa hedhi. Wastani huu utasema tu kwamba kwa ujumla unaingia hedhi baada ya siku ngapi lakini unaweza kubadilika muda wowote.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

20 Oktoba 2024, 06:51:51

Rejea za mada hii:

Apter D., et al. Follicular growth in relation to serum hormonal patterns in adolescent compared with adult menstrual cycles. Fertil Steril. 1987;47(1):82–88.

Fraser I.S., et al. Pituitary gonadotropins and ovarian function in adolescent dysfunctional uterine bleeding. J Clin Endocrinol Metab. 1973;37(3):407–414.

Groome N.P., et al. Measurement of dimeric inhibin B throughout the human menstrual cycle. J Clin Endocrinol Metab. 1996;81(4):1401–1405.

Hallberg L., et al. Menstrual blood loss--a population study. Variation at different ages and attempts to define normality. Acta Obstet Gynecol Scand. 1966;45(3):320–351.

Health line. Forget 28 days cycle. https://www.healthline.com/health-news/forget-28-day-cycle-womens-fertility-is-complicated. Imechukuliwa 20.10.2024

Lenton E.A., et al. Normal variation in the length of the follicular phase of the menstrual cycle: effect of chronological age. Br J Obstet Gynaecol. 1984;91(7):681–684.

Presser, H.B., Temporal data relating to the human menstrual cycle, in Biorhythms and Human Reproduction, M. Ferin, et al., Editors. 1974, John Wiley and Sons: New York. p. 145-160.

Sawetawan C., et al. Inhibin and activin differentially regulate androgen production and 17 alpha-hydroxylase expression in human ovarian thecal-like tumor cells. J Endocrinol. 1996;148(2):213–221.

Treloar A.E., et al. Variation of the human menstrual cycle through reproductive life. Int J Fertil. 1967;12(1 Pt 2):77–126.

Tsafriri, A., Local nonsteroidal regulators of ovarian function, in The physiology of reproduction, E. Knobil, J.D. Neill, and et al., Editors. 1994, Raven: New York. p. 817-860.

Vollman R.F., The Menstrual Cycle. 1977, WB Saunders: Philadelphia.

Welt C.K., et al. Control of follicle-stimulating hormone by estradiol and the inhibins: critical role of estradiol at the hypothalamus during the luteal-follicular transition. J Clin Endocrinol Metab. 2003;88(4):1766–1771.

bottom of page